Imeelezwa kuwa, makusanyo yameongezeka kufikia asilimia 93 katika kipindi cha miezi 9 katika ofisi ya madini Njombe.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Msafiri Mbibo wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Madini Mkoa wa Njombe.
“Nimefurahishwa na jinsi Ofisi ya Madini inavyoratibu shughuli zake na hasa ubunifu sahihi unaofanywa wa njia za kuongeza makusanyo,” amesema.
Aidha, amesisitiza watumishi kuendeleza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ili wavuke lengo baada ya kufunga mwaka wa fedha 2021/2022.
Akizungumzia ushirikiano, Mbibo amewaeleza kuwa, Wizara ya Madini itaendelea kushughulikia changamoto za watumishi zilizowasilishwa kwake ili kuongeza ufanisi wa kazi katika ofisi hiyo. Kwa upande mwingine, amewataka wafanye kazi kwa bidii ili Sekta ya Madini iongeze tija kwa Taifa.
Naye Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe Frederick Jirenga, ameahidi kutekeleza maelekezo yote kwa usahihi na kwa wakati na kushirikiana na watumishi ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wao.