***************************
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji imeitaka serikali kuwekeza nguvu zaidi katika kutoa elimu kwa umma juu ya udhibiti wa sumukuvu ili kupunguza madhara yanayosababishwa na sumukuvu.
Hayo yamesemwa leo Wilayani Kibaha,Mkoa wa Pwani na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji Mh.Dr. Christine Ishengoma katika ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa karantini na maabara ya Kituo cha udhibiti wa magonjwa ya kibailojia ya mimea (National Biocontrol Unit) chini ya mradi wa UDHIBITI WA SUMUKUVU.
“Tunaipongeza serikali kwa
Ujenzi wa maabara ya udhibiti wa magonjwa ya kibaolojia ya mimea,ambayo kukamilika kwake kutasaidia sana kupunguza matumizi ya kemikali kama viuatilifu katika mimea katika kudhibiti magonjwa na mashambulio ya wadudu waharibifu katika mimea.
Mkandarasi wa majengo haya lazima ahakikishe kwamba majengo haya yanakamilika kwa wakati na kwa ubora wa vigezo vya kimataifa vya maabara ya aina hii.
Aidha serikali ihakikishe inatoa elimu kwa umma na hasa kwa wakulima wadogo wadogo juu ya udhibiti wa sumukuvu katika mimea na kuelimisha wakulima juu ya matumizi ya wadudu marafiki katika kudhibiti magonjwa ya mimea”Alisema Dr.Ishengoma
Akitoa maelezo ya awali Naibu Waziri wa Kilimo Mh Anthony Mavunde ameishukuru Kamati ya Bunge kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia na kuishauri serikali katika masuala yahusuyo kilimo na kuahidi kuyafanyika kazi maelekezo yaliyotolewa.
Mh Mavunde aliongeza kwamba katika utekelezaji wa mradi wa huu UDHIBITI WA SUMUKUVU,serikali imeweka lengo la kuwafikia na kutoa elimu kwa wakulima 60,000,Maafisa Ugani 1351,Wafanyabiashara 5000 na Waandishi wa Habari 100 pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu kwa kufadhili shahada za Uzamivu(PhD) kwa wataalamu watano (5) na Shahada za Uzamili 19.
Katika mradi huu wa UDHIBITI WA SUMUKUVU pamoja na ujenzi wa Maabara ya utafiti kwenye Kituo cha Taifa cha udhibiti magonjwa ya mimea Kibaha pia utahusisha utekelezaji wa miradi mingine katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar itakayohusisha;
● Kujenga maghala 14 ya kuhifadhi mazao ya chakula;
● ujenzi wa kituo mahiri cha usimamizi wa mazao baada ya kuvuna (Post harvest Center of Excellency)
● Ujenzi wa Maabara Kuu ya Kilimo.