Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akiongea na Mkurugenzi wa Redio China Kimataifa , Ofisi ya Nairobi Bi. Du Shunfang (katikati) Machi 16, 2022 jijini Arusha ambapo walijadiliana namna Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) watakavyo shirikiana na Redio China Kimataifa ili kuendelea kukuza lugha adhimu ya Kiswahili duniani.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ongea na Mkurugenzi wa Redio China Kimataifa, Ofisi ya Nairobi Bi. Du Shunfang (wa pili kushoto) Machi 16, 2022 jijini Arusha.
*******************
Na Eleuteri Mangi, WUSM-Arusha
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema Serikali ya Tanzania ipo mstari wa mbele kushirikiana na Redio China Kimataifa ili kuendelea kukuza lugha adhimu ya Kiswahili duniani.
Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema hayo alipokutana na kufanya kikao Machi 16, 2022 na Mkurugenzi wa Redio China Kimataifa , Ofisi ya Nairobi Bi. Du Shunfang ambaye ni miongoni mwa washiriki wa Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Dunia linaloendelea katika Kituo cha Mikitano cha Kimataifa (AICC) jijini Arusha kwa siku tano kuanzia Machi 14-18, 2022.
“Tumeona tutumie fursa hii ya uwepo wako hapa nchini kwenye Kongamano hili ili tuone namna bora na maeneo ya ushirikiano katika kukuza na kuendeleza lugha aushi ya Kiswahili duniani kupitia Redio China Kimataifa” amesema Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu.
Katika mazungumzo yao, Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu na Mkurugenzi wa Redio China Kimataifa Bi. Du Shunfang wamekubaliana kuwa wataona namna bora ambayo Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) watatoa maudhi ya vipindi vya kukuza na kuendeleza Kiswahili nchini China na Redio China Kimataifa watatangaza na kusambaza maudhui hayo.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu ameongeza kuwa kuna haja ya kuwa na Kongamano la Kiswahili ambalo litafanyika mara moja kwa mwaka nchini China ili kuendelea kuongeza wigo wa kukuza lugha ya Kiswahili nchini humo na kutoa fursa ya watu wengi kushiriki na kujifunza istilahi, misemo, methali, nahau na maneno mengine ambayo yatatumika kulingana na muktadha na mazingira ya nchi hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Redio China Kimataifa, Ofisi ya Nairobi Bi. Du Shunfang amesema kuwa Kiswahili kina soko kubwa nchini China katika maeneo mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara, kufundisha katika shule na vyuo mbalimbali vinavyofundisha lugha ya Kiswahili kama somo na lugha ya kigeni kwa ajili ya biashara.
Katika kueneza Kiswahili nchini China, yeye ametafsiri vitabu sita vya Kiswahili kwenda lugha ya Kichina na Kichina kwenda Kiswahili na kuna watu wanafanya utafiti na kuandika vitabu vya Kiswahili na chanzo cha lugha ya Kiswahili ni Utamaduni.
“Mahitaji ya kufundisha lugha ya Kiswahili bado ni makubwa, kwa sasa lugha ya Kiswahili inafundishwa kupitia mashirika ya kimataifa na kuna taasisi tatu China zinafanya utafiti katika mambo ya Afrika ikiwemo Kiswahili” amesema Bi. Du Shunfang.
Bi. Du Shunfang amesema kuwa Redio China Kimataifa inawasikilizaji wengi kupitia mtandao wa facebook zaidi ya milioni mbili na kuongeza kuwa Wachina wote wanaokuja Afrika wanapenda kujifunza lugha ya Kiswahili na kuna wataalamu zaidi ya 200 huku lugha hiyo ikianza kufundishwa nchini humo tangu miaka ya 1960.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Tifa Bi. Consolata Mushi amesema Baraza hilo lltandaa vipindi maalumu vya kufundisha Kiswahili kwa wageni ambavyo vitarushwa kupitia Redio China Kimataifa.
Zaidi ya hayo, Bi. Consolata amesema kuwa Baraza katika vipindi vyake watakavyoandaa watatumia maneno rahisi ambayo yatasaidia watu wengi kujifunza lugha ya Kiswahili na hivyo lengo la kueneza lugha hiyo kimataifa kufikiwa na kuenea duniani ikizingatiwa chombo cha habari pamoja na mitandao ya kijamii ndiyo njia rahisi ya kuwafikia watu wengi kwa mara moja.