Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
KAMATI ya Bunge ya kudumu ya Nishati na Madini, imeiagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA ) pamoja na Wizara ya Nishati kuongeza usimamizi kwenye miradi ya REA Mkoani Pwani na nchi nzima kijumla ili ikamilike kwa wakati, ifikapo Desemba mwaka huu.
Aidha imeeleza, Serikali inaendelea kuhakikisha umeme unafika Vijijini na maeneo ya pembezoni ili kuinua uchumi na maendeleo katika maeneo hayo.
Wakitembelea baadhi ya miradi ya REA awamu ya III mzunguko wa pili, wilayani Mkuranga Mkoani Pwani, wajumbe wa kamati ya Nishati na madini ,iliyoambatana na timu ya REA, TANESCO na Wizara ya Nishati, wilayani Mkuranga Mkoani Pwani, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dustan Kitandula aliwataka wakandarasi wote nchini kukamilisha miradi hiyo kulingana na mkataba.
Alieleza, mradi wa REA awamu ya III mzunguko pili ulianza agost mwaka 2021 na unatakiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
“Tumekuja kufuatilia utekelezaji wa miradi tuliyoipitishia fedha mwaka uliopita kwa wilaya ya Mkuranga,tulipitisha Bilioni 8.1 kwa ajili ya Vijijini 43”
“Mkandarasi amejitahidi,Ila changamoto muda uliobaki Ni miezi Tisa ,muda huo ni mfupi,hatuna Shaka Kama miradi hataisha kwa wakati Lakini usimamizi na ufuatiliaji Ukilegalega tutajikuta wakandarasi wanaomba muda wa nyongeza”alifafanua Kitandula.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, January Makamba alisema wamepokea maelekezo na Nia ya Wizara na Serikali ni kuona mradi unanufaisha wananchi lengwa.
Makamba alisema, Serikali inatenga fedha nyingi na Rais Samia Suluhu Hassan amejipanga kufikisha umeme Vijijini na kuona matokeo ya chanya katika miradi inayopelekewa fedha .
Alielekeza,shule ya Makele kata ya Njianne ifikishiwe umeme ndani ya wiki mbili ili walimu na wanafunzi waweze kufanya majukumu yao ya kielimu vizuri.
Awali Mkurugenzi REA, Mhandisi Hassan Saidy akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme awamu ya III mzunguko wa pili, alisema vijiji 333 kati ya 442 vimepatiwa umeme kupitia miradi mbalimbali sawa na asilimia 75.
Vitongoji vilivyopatiwa umeme ni 1,050 kati ya 2,028 ambayo ni asilimia 52, vijiji 109 kati ya 442 sawa na asilimia 25 bado havijaunganishiwa.
Saidy alisema vijiji 89 kati ya 109 ambavyo bado havijaunganishiwa umeme vitapatiwa umeme katika mradi wa REA awamu ya III mzunguko wa pili ambao upo hatua ya utekelezaji.
Anaeleza mkandarasi China Railway CRCEBG anaendelea na utekelezaji wa mradi,na aliongeza mradi huo kupeleka umeme vijiji 89 visivyo na umeme utagharimu sh.Bilioni 37.4.
Michael Ngonyani kutoka Mercados Aries (mkandarasi),alisema watahakikisha wanatekeleza mradi kwa wakati licha ya changamoto wanazokabiliana nazo.
Ngonyani alieleza wanakabiliwa na changamoto ya Ununuzi wa vifaa gharama kupanda ,vifaa vinavyopatikana nje ya nchi kutofika kwa wakati wakati wa Covid 19 pia upatikanaji wa nguzo kuchelewa.
Diwani kata ya Njianne Ally Mbwera na mkazi wa Njianne ,mzee Omary Ally walishukuru Serikali kwa kufikisha umeme Vijijini hususan vijiji vya kata hiyo ikiwemo Ming’ombe na Makele.
Waliomba usambazaji uongezwe maeneo yaliyobakia na Taasisi za umma na Taasisi za kidini.