Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso (wa pili kulia) akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo kukagua ujenzi wa mnara wa mawasiliano ya simu wa Vodacom kwa ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) katika kijiji cha Nyampande wilayani Sengerema
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kukagua mnara wa mawasiliano ya simu wa Vodacom uliojengwa kwa ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) katika Kijiji cha Nyampande wilayani Sengerema.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakitembelea na kukagua miundombinu ya mawasiliano, ikiwamo mnara wa mawasiliano wa kijiji cha Nyampande Sengerema, Kituo cha huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Anwani za Makazi na Postikodi jijini Mwanza, aliyeambatana nao ni Mhe. Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (wa pili kushoto) akiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mohammed Abdulla wakati wakivuka daraja la Kigongo- Busisi alimaarufu daraja la Magufuli akitokea jijini Mwanza kuelekea Kijiji cha Nyampande kukagua ujenzi wa mnara wa mawasiliano ya simu wa Vodacom kwa ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) katika kijiji cha Nyampande wilayani Sengerema
***********************
- Shilingi Bilioni 5.4 Zatumika Kujenga Minara 40 Mwanza
- Zaidi ya Wananchi 6,000 wa Kata ya Nyampande, Sengerema Wapata Mawasiliano
- Wananchi 2,500 kati ya 6,000 wanatumia Data kupitia Mnara wa Nyampande
- Asilimia 99 ya Mnara Uliojengwa Nyampande Unatumiwa na Wananchi
- Kamati Yakagua na Kupongeza Utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi
Na Prisca Ulomi, WHMTH, Mwanza
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhishwa na jitihada za Serikali za kupeleka mawasiliano kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso wakati wa ziara ya Kamati yake mkoani humo ya kukagua miradi ya huduma za mawasiliano iliyotekelezwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa wananchi wa Mkoa huo leo tarehe 16 Machi, 2022 ambapo kamati hiyo imekagua ujenzi wa mnara wa mawasiliano wa Nyampande na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye eneo hilo; kufuatilia utekelezaji wa operesheni ya anwani za makazi; na kukagua mitambo ya Mkongo wa Mawasiliano ya Taifa
Mhe. Kakoso amesema kuwa Kamati imeridhishwa na ujenzi wa minara 40 ya simu unaoendelea mkoani humo na wanaishukuru Wizara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kupeleka mawasiliano kwa wananchi kwenye maeneo ambayo hayakuwa na mvuto wa kibiashara na amewataka wananchi kutambua kuwa matokeo haya yanatokana na Wabunge wa maeneo haya ambao ni wawakilishi wa wananchi kuhakikisha kuwa Serikali inajenga minara hiyo na faida inayopatikana itumike kutengeneza uchumi na huduma za maendeleo ya jamii kama vile kujenga madarasa, zahanati ili wananchi wanufaike
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ameieleza Kamati kuwa ujenzi wa mnara huo wa mawasiliano umefanyika kwa ubia kati ya Serikali na kampuni ya simu ya Vodacom ambapo Serikali imewapatia fedha Vodacom kama chachu ili waweze kujenga mnara huo na amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel kwa utekelezaji mzuri unaoendelea wa operesheni ya anwani za makazi na kuwa chachu kwa wengine
Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mshiba amesema kuwa ujenzi wa minara 18 imekamilika; ujenzi wa minara 22 utakamilika mwezi Juni mwaka huu 2022 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5.4 kitatumika kujenga minara hiyo katika mkoa wa Mwanza ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni wanapata huduma za mawasiliano
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Sitholizwe Mdlalose amesema kuwa kampuni yake iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kujenga minara ili wananchi wapate huduma za mawasiliano ya uhakika
Mhe. Mhandisi Gabriel amesema kuwa utekelezaji wa operesheni ya anwani za makazi unaendelea vizuri ambapo jumla ya nyumba 643,298 kati ya nyumba 551,554 zimewekewa namba sawa na asilimia 118.5; jumla ya anwani 103,558 zimesajiliwa katika mfumo wa NAPA sawa na asilimia 15.8; na nguzo zinazoonesha majina ya barabara 6,007 zimewekwa kati ya nguzo 65,384 sawa na asilimia 9.1 ambapo elimu inaendelea kutolewa kwa wadau ili waweze kushiriki kikamilifu utekelezaji wa mfumo huu na ukamilishwe ifikapo mwezi Mei, 2022.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari