**************
Baadhi ya Wakuza Mitaala wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) leo tarehe 14/3/2022 wamepata nafasi ya kupokea maoni ya wadau wanajihusisha na masuala ya mtoto njiti.
Mkutano huo unaofanyika katika hoteli ya Nashera mjini Morogoro ni muendelezo wa zoezi la kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali nchini ili kuboresha Mitaala ya Elimu nchini kuanzia ngazi ya Awali,Msingi,Sekondari na Ualimu.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa DORIS MOLLEL FOUNDATION, Bi.Doris Molel amesema kuwa elimu ya afya kwa mama mja mzito ambaye anaweza kujifungua mtoto njiti ni muhimu ikawekwa kwenye mitaala kwasababu itasaidia sana katika kupunguza tatizo hili.
“Hii elimu ikiwekwa kwenye mitaala ya elimu ya Msingi hadi Sekondari itasaidia sana katika uelewa wa watoto wanaozaliwa njiti” amesema Doris Molel.
Kwa upande wake , Mkurugenzi wa Ubunifu na Ukuzaji Mitaala ,Dkt.Godson Lema ameelezea kuwa masuala ya elimu kuhusiana na mtoto njiti itazingatiwa katika Mitaala inayoboreshwa .Hii itasaidia kutoa uelewa kwa jamii kuhusu sababu za mtoto kuzaliwa njiti na namna ya kuwalea.