Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga akitoa maelekezo kwa mmoja wa waandisi wanaosimamia mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Ikungi.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya Wizara, VETA na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakati Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga alipofanya ziara yaa kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha VETA Wilaya ya Ikungi.
Mmoja wa mafundi wanaoshiriki katika ujenzi wa Chuo cha VETA Wilaya ya Ikungi akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro, viongozi wa VETA na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi waliofika kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha VETA Ikungi.
Muonekano wa moja ya jengo linaloendelea kujengwa katika Chuo cha VETA Ikungi
………………………………..
Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) imetakiwa kukamilisha Mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Wilaya ya Ikungi ifikapo Aprili 4, 2022 ili kuwezesha udahili wa wanafunzi kuanza Juni mwaka huu.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga wilayani Ikungi baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambapo amesema Chuo hicho ni miongoni ya vyuo 25 vinavyojengwa katika wilaya mbalimbali nchini na mpaka sasa zaidi ya Shilingi bilioni 2.4 zimeshatolewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chuo hicho.
Mhe. Kipanga amesema mradi huo ulioanza mwaka fedha 2019/20 ulisimama kwa muda wa mwaka mmoja kutoka na changamoto ya usimamizi iliyopelekea kukabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambapo baadaye ulirudishwa tena VETA kutokana na taratibu za kimfumo ambazo hazikuwezesha Halmashauri hiyo kusimamia ujenzi huo.
“Mradi huu ulisitishwa ili kufanya tathmini ya namna fedha na vifaa vingine vilivyotumika na tathmini hiyo ilionyesha ukiukaji mkubwa wa taratibu za matumizi ya fedha ambapo wote waliohusika tayari wameshachukuliwa hatua za kiutumishi na dhamira yetu ya kuona unakamilika ifikapo aprili 4 ipo palepale,” amesisitiza Naibu Waziri.
Aidha, Mhe. Kipanga ameongeza kuwa katika fedha za nafuu ya UVIKO 19 Wizara ilipata zaidi ya Shilingi milioni 64 ambazo zitatumika maeneo mbalimbali, huku Shilingi bilioni 20 zikitengwa kwa ajili ya kukamilisha vyuo 25 vya VETA vya Wilaya na Shilingi bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Mikoa ya Njombe Rukwa, Geita na Simiyu.
Ameongeza kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari ameshaidhinisha Shilingi bilioni 8.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika vyuo vyote vipya vya VETA vinavyojengwa.
Mhe. Kipanga ameongeza kuwa jitihada hizi zote za kuongeza vyuo vya VETA zinalenga kuwezesha vijana wanaomaliza ngazi mbalimbali za elimu na hawana nia na kuendelea na masomo waweze kujiunga na vyuo hivyo ili wapate ujuzi na umahiri katika ufundi utakaowawezesha kujiajiri ama kuajiriwa na hatimaye kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa viwanda.
Mhe. Kipanga amesema kukamilika kwa vyuo vyote 25 vitawezesha kudhaili zaidi ya wanafunzi 25,000 kwa kozi za muda mfupi na mrefu ambapo kwa kozi za muda mrefu inategemewa kudahili wanafunzi 12,500.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro ameishukuru Wizara ya Elimu kwa kuweka uangalizi wa karibu ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuongeza kuwa Wilaya ya Ikungi inauhitaji mradi huo ili kuwezesha vijana wa Wilaya hiyo kupata ujuzi na umahiri utakaowawezesha kushiriki katika miradi ya kimkakati.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu amemhakikishia Naibu Waziri kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati kwa kuwa mahitaji yote yanayohitajika kwa ajili ya ujenzi yapo na kwamba wamejipanga kufanya kazi usiku na mchana.