Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKOA wa Pwani umeanza operesheni ya kukamata wahamiaji haramu kwenye mkoa huo,ili kupunguza ama kuondoa wimbi la wahamiaji hao wanaoingia kupitia njia za panya pasipo kufuata sheria.
Operesheni hiyo ,Ni utekelezaji wa agizo la Inspekta Jenerali wa Uhamiaji Nchini Anna Makakala , alilolitoa ili kusaidia kuchunguza na kubaini wahamiaji haramu na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ,kuchukuliwa hatua stahiki.
Akizungumza na maofisa Uhamiaji wa mkoa huo, mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alisema zoezi hilo litakuwa zoezi maalumu ambalo litaisha Machi 23 mwaka huu.
Vilevile, alieleza zoezi hilo litagusa kwenye maeneo ya uwekezaji hivyo wawekezaji wanapaswa kutoa ushirikiano ili kufanikisha.
“Kwa kuwa taratibu za kuishi nchini zipo ni vema wageni wakazifuata kwani hakuna sababu ya wageni kuingia au kuishi kinyume cha sheria,”alifafanua.
Naye ofisa Uhamiaji wa mkoa wa Pwani Omary Hassan alisema kuwa baadhi ya wahamiaji haramu hutafuta fursa za ajira hasa wanaotoka pembe ya Afrika ikiwemo Ethiopia huwa wanapita kwenda Kusini mwa Afrika kutafuta maisha.
Alisema kuwa operesheni hiyo itapita maeneo mbalimbali hasa ikizingatiwa mkoa huo una sehemu nyingi za barabara kuu za mikoa mbalimbali ambayo inapita mkoa wa Pwani na sehemu ya bahari.