Mtambo wa umeme wa jua uliokamilika kujengwa na RUWASA Wilaya ya Sumbawanga katika chanzo cha maji kwenye mradi wa kijiji cha Mponda kata ya Majengo Manispaa ya Sumbawanga ambapo watu 1,768 wananufaika.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Sumbawanga Mhandisi Jonas Maganga akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) akiwa juu ya tanki la maji katika kijiji cha Kisa Kata ya Milepa ambapo mradi huo umekamilika na watu 6,901 wananufaika.
Meneja wa Ruwasa Sumbawanga Mhandisi Jonas Maganga akipanda kukagua tanki la kuhifadhia maji lililokamilika kujengwa na Ruwasa Sumbawanga katika kijiji cha Kisa kata ya Milepa lenye uwezo wa kuhifadhi lita 225,000 za maji juzi wakati wa ziara ya waandishi wa habari ikiwa ni maandalizi ya Wiki ya Maji.
Wananchi wa Kijiji cha Nankanga wilaya ya Sumbawanga wakipata huduma ya maji kufuatia Ruwasa kukamilisha mradi huo hivi karibuni .
Wananchi wa kijiji cha Lwanji kata ya Mtowisa wilaya ya Sumbawanga wakichota maji kufuatia mradi kukamilika baada ya serikali kuipatia Ruwasa fedha katika mwaka 2021/22.
Mhandisi Jonas Maganga ambaye ni Meneja wa Ruwasa Sumbawanga akikagua koki ya maji katika kijiji cha Kipenzi kata ya Mfinga wakati wa ukaguzi wa mradi huo juzi kufuatia kukamilika kwake.
……………………………………….
Na. OMM Rukwa
Katika kuadhimisha mwaka mmoja wa serikali ya Awamu ya Sita, wananchi wa Sumbawanga wamefanikiwa kupata uhakika wa maji safi na salama baada ya Ruwasa wilaya ya Sumbawanga kukamilisha miradi 14.
Akizungumza na waandishi wa habari jana (12 Machi,2022) Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Sumbawanga Mhandisi Jonas Maganga alisema jumla ya miradi 14 imekamilika na kuanza kutoa maji mwaka 2021/2022.
Mhandisi huyo aliongeza kusema serikali ya Awamu ya Sita imewawezesha kupata fedha ambapo wamekamilisha miradi 14 ya zamani na kujenga miradi mipya minne hatua yaliyowezesha watu 63,000 kupata maji safi katika vijiji vya Sumbawanga.
“Katika mwaka 2021/22 serikali ilitupatia shilingi Bilioni 2.8 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji wilaya ya Sumbawanga ambapo vijiji 114 vya halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na vijiji 24 vya Manispaa ya Sumbawanga vimenufaika” alisema Mhandisi Maganga.
Mhandisi Maganga alisema kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 1.8 kwa miradi nane (6) mpango wa matokeo (BfR), Shilingi Milioni 600 kwa ajili ya miradi minne (4) ya Lipa kwa matokeo ya haraka (PbR) na shilingi Milioni 400 toka Serikali Kuu
Katika hatua nyingine Mhandisi Maganga alisema mafanikio mengine ni kupitia jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan, Wakala ulipatiwa shilingi Milioni 909 za Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano ya UVIKO-19 kwa ajili ya miradi ya maji kwenye vijiji viwili.
Kati ya fedha hizo za UVIKO-19 Ruwasa Sumbawanga inatekeleza mradi wa maji wa kijiji cha Mkwiro kwa gharama ya shilingi Milioni 495 ambapo utanufaisha wananchi 2,444 na kuwa kazi ya ujenzi wa chanzo imeanza na usambazaji mabomba yenye urefu wa kilometa 8 na vituo vya kuchotea maji 11 unaendelea na umefikia asilimia 15.
Mradi mwingine unaonufaika na fedha hizo ni wa kijiji cha Mwenzusi Manispaa ya Sumbawanga ambapo jumla ya shilingi Milioni 497 zinatumika kukarabati chanzo cha maji, kununua pampu, kuweka mfumo wa umeme jua na kujenga vituo 16 vya kuchotea maji.
“ Mradi huu wa Mwenzusi utakamilika mwezi Juni mwaka huu ambapo jumla ya watu 7,599 pamoja na taasisi nne za serikali zitanufaika hivyo Ruwasa tunamshuru sana Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuithamini sekta ya maji na kuwezesha ipate fedha nyingi” alisisitiza Mhandisi Maganga.
Kuhusu changamoto za Ruwasa Mhandisi Maganga alitaja kuwa ni pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya maji kupitia shughuli za binadamu ambazo kwa Sumbawanga ni kilimo na Mifugo.
Kwa Sumbawanga ambayo ina vyanzo vya maji ya mseleleko Mhandisi huyo alisema hali ya uchafuzi wa vyanzo vya maji inapelekea kipindi cha masika maji kuwa na uchafu na matope hatua inayoleta manung’uniko toka kwa wateja.
Ikiwa ni maandalizi ya Wiki ya Maji Kitaifa mwaka huu itakayoanza Machi 16 hadi 22 , Waandishi wa habari walifanikiwa kufanya ziara katika vijiji vya Mkwiro, Nankanga, Milepa na Lwanji vya Sumbawanga kuangalia utekelezaji wa miradi hiyo.
Akieleza faida za mradi ya maji Florenci Magambo ambaye ni Mtendaji wa Kijiji Nkwilo Sumbawanga alisema upatikanaji wa maji utasaidia kuondoa migogoro ndani ya familia hususan kwa akina mama na kuomba mkandarasi akamilishe mradi huo kwa haraka.
Mkazi kijiji cha Lwanji Andrew Kasamnya alisema changamoto za maji iliyokuwepo miaka mingi ya ukosefu wa maji sasa imekwisha baada ya maji kuanza kutoka kwa kazi ya Ruwasa
Naye Daniel Mwendapole mkazi wa Kijiji cha Mkwilo alisema sasa kuna uhakika wa maji na alishukuru serikali kwa kufanikisha miradi hiyo ya maji hivyo kuwasaidia kupunguza magonjwa.
Akizungumza kuhusu mikakati wa RUWASA kudhibiti uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji Msimamizi wa Vyombo vya Watumiaji Huduma za Maji Ngazi ya Jamii Kumbuka Daudi alisema tayari wanashirikiana na serikali za vijiji na kata kutoa elimu ya ulinzi wa vyanzo vya maji kwa kuacha kulima pia kuchoma moto Misitu.
Kumbuka alisema katika Wiki ya maji mwaka huu 2022 wamepanga kufanya mafunzo shirikishi na viongozi wa vijiji 29 vya Sumbawanga wakiwemo watendaji wa vijiji, kata na madiwani ili wasaidie udhibiti wa uharibifu wa vyanzo vya maji.
Ruwasa wilaya ya Sumbawanga inahudumia vijiji 114 vya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na vijiji 24 vya Manispaa huku kukiwa na vijiji 38 bado havijapata huduma za maji ambapo hali ya upatikanaji maji umefikia asilimia 68 mjini na asilimia 50 vijijini.