Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji nchini, Bw. Koenraad Goekint, mara baada ya kikao kilichofanyika Wizarani, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba (wa pili kulia) na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji nchini, Bw. Koenraad Goekint (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga (Kushoto), na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban (Kulia), jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, akizungumza wakati wa kikao na ujumbe kutoka Ubelgiji, jijini Dodoma. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Nyamanga, na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji nchini Tanzania, Bw. Koenraad Goekint, akizungumza wakati ujumbe wa nchi hiyo ulipofanya kikao na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Kushoto ni Mshauri wa Mwakilishi Mkazi wa Ubelgiji nchini Bw. Lokota Ndibalema, jijini Dodoma.
Balozi wa Tanzania Nchini Ubelgiji Mhe. Jestsas Nyamanga, akizungumza wakati wa kikao na ujumbe kutoka Ubelgiji. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba na kulia ni Mkuu wa Idara ya Ulaya na Marekani, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Swahiba Mndeme, anayesimamia Bara la Ulaya na Amerika, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Shaaban, akizungumza jambo wakati wa kikao na ujumbe kutoka nchini Ubelgiji, jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba na kushoto ni Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Patrick Pima.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba na Ujumbe wa Ubelgiji ukiongozwa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji nchini, Bw. Koenraad Goekint, wakiwa katika kikao cha pamoja, Jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM- Dodoma)
********************
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
SERIKALI ya Ubelgiji imeahidi kuipatia Tanzania Euro milioni 25 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 62, kwa ajili ya kutekeleza program mpya ya maendeleo ya miaka mitano katika sekta ya elimu, inayotarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2023 hadi mwaka 2027, katika mkoa wa Kigoma.
Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji-ENABEL, Bw. Koenrad Goekint aliyeongoza ujumbe wa watu 7 kutoka nchini Ubelgiji walipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu MKuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba.
Bw. Goekint alisema kuwa Programu hiyo itajikita katika kuendeleza sekta ya elimu kwa kuangazia maeneo ya ukuzaji ujuzi wa ajira na utaalam kwa vijana hususan masuala ya uanagezi na ujasiriamali kwa lengo la kuzalisha ajira, kuimarisha usawa wa kijinsia kwa kukuza zaidi ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za maendeleo na kuboresha masuala ya usawa wa kijinsia
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, amelishukuru Shirika la Maendeleo la Ubelgiji-ENABEL kwa kuja na Program hiyo itakayotoa matokeo mazuri kwa kugusa maisha ya wananchi wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo.
“Program hii itakayotekelezwa mkoani Kigoma itagusa maenneo ya kipaumbele yaliyoainishwa kwenye utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26), wenye lengo la kuboresha huduma za jamii, maisha ya watu na elimu ni moja ya maeneo hayo” alisema Bw. Tutuba.
Bw. Tutuba aliiomba Serikali ya Ubelgiji kupitia Shirika lake la Maendeleo-ENABEL, kuangalia uwezekano wa kuongeza maeneo mengine ya kimkakati ya kuboresha maisha ya wananchi ikiwemo huduma za afya na maji kwani wanawake ndio walengwa wakuu na ndio wanaokabiliana na changamoto ya uhaba wa maji.
Aidha, Bw. Tutuba aliishauri Serikali ya Ubelgiji kupitia Shirika hilo kutekeleza mradi kama huo kwa upande wa Zanzibar ili kuwawezesha wananchi wa Visiwa hivyo kufurahia matunda mazuri ya uhusiano mwema uliopo kati ya Tanzania na Ubelgiji.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania Nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Nyamanga, alisema kuwa kufanyika kwa ziara hii ni ishara nzuri ya kuendelea kuimarika kwa uhusiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Ubelgiji na ni matokeo chanya ya ziara ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipofanya ziara ya kikazi nchini Ubelgiji tarehe 14 hadi 19 Februari 2022.
Akiwa nchini Ubelgiji, Mheshimiwa Rais alikutana kwa mazungumzo na viongozi mbalimbali akiwemo Mheshimiwa Alexander De Croo, Waziri Mkuu wa Ubelgiji ambapo Viongozi hao walikubaliana kuweka mikakati ya kufanyika kwa majadiliano ya programu ya maendeleo na kuhakikisha kuwa mchakato wa maandalizi unakamilishwa kwa wakati.
Balozi Nyamanga alifafanua kuwa Tanzania imeingia katika orodha ya nchi 15 pekee duniani ambazo Ubelgiji inaendesha program kama hizo jambo ambalo ni ishara ya mafanikio makubwa ya uhusiano uliopo kati ya nchi hizi mbili na alitoa wito kwa taasisi zote zitakazo kutana na ujumbe huo wa Ubelgiji hapa nchini kuweka kipaumbele mahitaji ya nchi katika eneo husika.
Ujumbe huo Shirika la Maendeleo la Ubelgiji-ENABEL unajumuisha watu saba na upo nchini kuanzia tarehe 7 hadi 18 Machi 2022, ambapo watafanya mazungumzo na Viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi za Serikali kuhusu maandalizi ya programu mpya ya ushirikiano.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban, Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga, na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swahiba Mndeme.