WAZIRI wa Madini Dk.Doto Biteko,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo March 10,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.
WAZIRI wa Madini Dk.Doto Biteko,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo March 10,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.
WAANDISHI wa Habari wakifatikia hotuba ya Waziri wa Madini Dk.Doto Biteko,leo March 10,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia
…………………………………………
Na Alex Sonna _DODOMA
WIZARA ya Madini imetaja mafanikio nane ambayo imeyapata katika kipindi cha mwaka mmoja wa awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,ikiwemo kusaidia kuongezeka kwa Pato la Taifa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo March 10,2022 jijini Dodoma wakati akitaja mafanikio hayo,,Waziri wa Wizara hiyo,Dotto Biteko amesema chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka kutoka robo moja ya mwaka hadi nyingine.
MCHANGO WA MADINI KATIKA PATO LA TAIFA WAONGEZEKA .
Amesema katika kipindi cha Januari – Septemba, 2021 wastani wa mchango wa sekta hii umekua hadi kufikia asilimia 7.3 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.
Aidha, katika robo ya tatu (Julai – Septemba) mwaka 2021, mchango wa sekta ya madini umeongezeka hadi kufikia asilimia 7.9 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 7.3 ya Pato la Taifa katika kipindi kama hicho mwaka 2020.
“Matokeo haya yanaakisi dhamira ya Serikali kuhakikisha sekta hii inaimarika na kuweza kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 kama ilivyotangazwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa na Mpango wa Maendeleo,”amesema.
MAUZO SHILINGI TRILIONI 8.3
Amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa serikali ya awamu ya sita sekta ya madini imeweka historia kwa kushuhudia mauzo ya moja kwa moja yenye thamani ya Shilingi Trilioni 8.3 kutokana na mauzo ya madini ya aina mbalimbali.
Amesema mauzo hayo yanatokana na madini ya dhahabu, fedha, shaba, makaa ya mawe,kinywe, madini ya vito na madini ya ujenzi na viwandani.
MADUHULI YA SHILINGI BILIONI 597.53
Waziri Biteko amesema kutokana na biashara ya madini hayo, Wizara imekusanya Shilingi Bilioni 597.53 kama maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa kupitia wizara hiyo.
Vile vile, ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za madini umekuwa kutoka asilimia 48 hadi asilimia 63 na hivyo kuongeza thamani ya huduma migodini kufikia thamani ya Dola za Marekani Milioni 579.3 sawa na Shilingi Trilioni 1.33 kutokana na huduma zilizotolewa migodini.
“Kwa sasa Wizara imeongeza usimamizi kwenye madini ya ujenzi na viwandani ambapo tayari mifumo ya kielekronik imeanza kutumika katika usimamizi wa mapato ya Serikali yatokanayo na madini hayo.
Amesema katika juhudi za kusimamia upatikanaji wa mapato kutokana na madini ya ujenzi na viwandani, Wizara ya Madini imeanza ushirikiano na Wizara ya TAMISEMI ili kuweza kuwafikia wananchi wanaotumia madini hayo waweze kuchangia fedha zitokanazo na shughuli za uchimbaji.
WACHIMBAJI WADOGO
Aidha,Waziri huyo amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhesimiwa Samia Suluhu Hasan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia na kuhakikisha wachimbaji wadogo wanashiriki kikamilifu na kwa ufanisi kwenye uzalishaji madini hapa nchini.
Amesema katika usimamizi huo, kwa sasa wachimbaji wadogo wanachangia zaidi ya asilimia 30 kwenye mapato yatokanayo na madini.
“Kiasi hiki ni cha juu ikilinganishwa na kiasi kidogo (asilimia 4 kabla ya marekebisho ya Sheria) kilichokuwa kikichangiwa na kundi hili muhimu katika Sekta ya Madini,”amesema.
Amesema mafanikio hayo ni juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Mheshimiwa Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Tanzania katika kuhakiksha wananchi wa kipato cha chini wanashiriki kwenye shughuli za madini na kunufaika na rasilimali za madini.
“Mchango huu wa wachimbaji Wadogo kwenye Sekta ya Madini unatokana na juhudi za Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha huduma muhimu kwa wachimbaji kama masoko zinapatikana,”amesema.
Amesema hadi sasa kuna masoko 44 na vituo vidogo vya kununulia madini ya dhahabu 70 ambapo amedai masoko hayo na vituo vya kununulia dhahabu vimeongeza uaminifu kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa biashara sasa inafanyika kwa uwazi na uaminifu zaidi.
MASOKO YAZIVUTIA BENK
Waziri Biteko amesema uwepo wa masoko umeongeza imani kwa Taasisi za fedha katika kutoa
huduma za kifedha kwa wachimbaji Wadogo.
Amezitaja Taasisi hizo ni mabenki ya NMB Bank; CRDB Bank; NBC Bank; Stanbic Bank; Azania Bank, Ecobank; and Standard Chartered Bank.
Amesema Kwa sasa mabenki ya NMB, CRDB yameanza kutoa mikopo kwa wachimbaji madini ambapo ameipongeza Benki hiyo.
“Hii ni dalili nzuri na yakutia moyo katika maendeleo ya Sekta ya Madini na nchi yetu.
LESENI 8,172 ZATOLEWA
Amesema wameshuhudia utoaji wa leseni mbalimbali kwenye shughuli za madini ukiongezeka ambapo jumla ya leseni 8,172 zimetolewa, kati ya leseni hizo, leseni 5,937 ni za uchimbaji mdogo wa madini (Primary Mining Lecence), leseni 282 ni za utafutaji wa madini (Prospecting Licence).
“Leseni 5 ni za uchimbaji wa kati wa madini (Mining Licence); leseni 2 ni za uchimbaji mkubwa wa madini (Special Mining Licence); leseni 49 ni za uchenjuaji wa madini (Processing Licence); leseni 2 ni za usafishaji wa madini (Refinery Licence).
“Leseni 1,531 ni za biashara ndogo ya madini (Broker Licence) na leseni 364 kubwa za biashara ya madini (Dealer Licence) zilitolewa kwa wawekezaji na wananchi, ikilinganishwa na jumla ya leseni 6,334 zilizotolewa katika kipindi cha kuanzia Machi 2020 mpaka hadi Februari 2021,amesema.
Amesema kati ya leseni zilizotolewa, takribani leseni 6 zenye uwekezaji mkubwa na kati zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji miradi hiyo.
Ameitaja Miradi ambayo ipo tayari kuanza shughuli za uzalishaji ni ule wa Uchimbaji dhahabu wa Shanta Singida, mgodi wa Jumbo Lindi wa Uchimbaji Madini ya Kinywe (graphite) ambayo ipo katika hatua za ujenzi wa miundo mbinu, mgodi wa Tembo Lickel ambao umepata leseni kubwa ya uchimbaji madini ya Nickel.
Miradi mingine ni ule wa Nyanzaga ambao baada ya kusainiwa makubaliano umeshaanza shughuli za ujenzi wa mgodi.
Aidha, kati ya leseni nne za Usafishaji madini (refining) tayari leseni tatu zimekamilisha ujenzi wa miundombinu ya Usafishaji ambapo Refinery ya Mwanza imeshaanza shughuli za usafishaji madini ya dhahabu baada ya Mheshimiwa Rais kufungua mradi huo mkoani Mwanza mwezi Juni, mwaka 2021.
SERIKALI YASAINI MIKATABA MIPYA MINNE
Amesema katika mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani, kwa mara ya kwanza katika historia ya Sekta ya Madini, Serikali ilifanikiwa kusaini mikataba mipya minne ya uchimbaji na uanzishwaji wa migodi mikubwa na ya kati ya madini kwa wakati mmoja.
“Ilikuwa tarehe 13 Desemba, 2021 ambapo dunia ilishuhudia Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na yeyé mwenyewe akiwepo kwenye tukio, ikisaini mikataba ya uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani milioni 735.79,”amesema.
Amesema Mikataba hiyo ilihusisha uchimbaji wa madini muhimu ya viwandani yanayotokana na mchanga wa baharini, madini ya dhahabu, almasi na madini ya kinywe (Graphite).
TOZO
Waziri Biteko amesema Juhudi mbalimbali zimefanyika kuwapunguzia adha za tozo zisizokuwa na tija kwa wananchi na wawekezaji katika sekta ya madini.
Amesema Marekebisho yamefanyika katika Sheria ya Madini, Sura 123 kwa vipengele ambavyo vilikuwa vinaleta mkwamo katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.
Waziri huyo amesema Tume ya Madini sasa inatoa leseni ndogo za biashara ya madini ya ujenzi na ya viwandani ambazo zitachochea na kuhamasisha wananchi kushiki kwenye uchimbaji na biashara ya madini haya na hivyo kuongeza wigo wa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia madini ujenzi na viwandani.
Pia, marekebisho mengine ya kisheria yaliyofanyika ni pamoja na kuruhusu Tume ya Madini kuruhusu uingizwaji wa madini kutoka nje ya nchi kuuzwa katika masoko ya ndani bila kutozwa VAT.