Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula (mwenye ushungi mweupe) akiongoza timu ya Menejimenti ya Wizara hiyo kuangalia eneo la kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Wizara katika mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma wakati walipokabidhiwa rasmi kiwanja hicho na mratibu wa ujenzi wa mji wa Serikali.
Mratibu wa Ujenzi wa mji wa Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Meshack Bandawe akimuonesha Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula, pamoja na timu ya Menejimenti eneo la Kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Wizara hiyo mpya katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Picha zote na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM
………………………………………………..
Na WMJJWM, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amewaomba Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) kuharakisha taratibu za kupata mchoro wa jengo la Ofisi za Wizara hiyo ili ujenzi uanze mapema.
Dkt. Chaula ametoa kauli hiyo
wakati akipokea kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Wizara, katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma tangu kuundwa kwa Wizara hiyo mpya ambapo kabla ilikuwa ni sehemu ya Wizara ya Afya.
Amesema TBA ifanye jukumu lake la kuhakikisha mchakato wa ujenzi unakamilika kwa wakati hivyo kuwezesha Wizara kuendelea kuhudumia wananchi kwa sababu inagusa makundi yote katika jamii ikiwemo makundi maalum.
“Kikubwa tunakimbizana na muda, kwa hiyo tumeshakabidhiwa eneo hili, hivyo wenzetu wa TBA watoe michoro ili ujenzi uanze kwani Wizara hii ni mtambuka” amesema Dkt. Chaula
Kwa upande wake, Mratibu wa ujenzi wa Mji wa Serikali Meshack Bandawe amesema kutokana na mahitaji ya Wizara hiyo kwa ukubwa wake kulikuwa na umuhimu wa kuwa na eneo lake na jengo kamili ili kurahisisha shughuli zake na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi ili kukidhi mahitaji ya Serikali kwa miaka ijayo.
“Kwa hatua hii tunatarajia jengo la Wizara hii litakuwa miongoni mwa majengo 25 yatakayojengwa hapa Mtumba, mara baada ya taratibu za kimamlaka kukamilika” amesisitiza Bandawe.
Naye Msanifu majengo kutoka TBA Ngh’olo Weja amesema TBA itatahakikisha mchoro wa majengo hayo, unakamilika mapema kwa kufuata sheria pamoja na taratibu zote za kumpata mkandarasi.