**********************
NJOMBE
Wafanyabiashara wawili kati ya sita wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mfawidhi wilaya ya Njombe kwa tuhuma za makosa ya kutotoa risiti sahihi za kielektroniki EFD kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
TAARIFA YA JOCTAN MYEFU KUTOKA NJOMBE
Wakisomewa mashitaka hayo ya kesi Namba 17 ya mwaka 2022 inayomkabili mfanyabiashara Raphael Ndelwa mkazi wa Njombe mjini na Frank Mbwilo anayekabiliwa na kesi namba 18 ya mwaka 2022 ambaye pia ni mkazi wa Njombe mjini,
Mwanasheria wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Athuman Mruma akisaidia na wanasheria wa Serikali Andrew Mandwa na Paul Ngonyani anasema mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Njombe Mheshimiwa Isack Mlowe kuwa mshitakiwa Ndelwa amefikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kutotoa risiti sahihi kwa mteja wake wakati alipouza bidhaa yenye thamani ya shilingi laki moja kinyume na kifungu cha sheria namba 86 kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya usimamizi wa kodi sura namba 438 iliyorejewa mwaka 2019.
Kuhusu mshitakiwa Mbwilo mwanasheria wa TRA, Mruma amesema mnamo Februari 8 mwaka huu katika mtaa wa Kwivaha mjini Njombe mfanyabishara huyo aliuza bidhaa yenye thamani ya shilingi elfu kumi na moja na miatano kwa mteja wake bila kutoa risiti ya EFD ikiwa ni kinyume na kifungu cha sheria namba 86 kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya usimamizi wa kodi sura namba 438 iliyorejewa mwaka 2019.
Hata hivyo wafanyabiashara wengine ambao wameshitakiwa kwa makosa ya kutotoa risiti ni pamoja na Zadek Ilomo, Adelhard Mgeni, Popati Mtenzi na Ibrahim Chengula ambao hawakuweza kufika mahakamani na kisha Mahakama kuamua kutoa hati ya wito wa kuitwa mahakamani hapo haraka iwezekanavyo ili kujibu tuhuma wanazokabiliwa nazo.
Kufuatia kutajwa kwa kesi hizo hakimu anasema dhamana yao iko wazi ambapo washitakiwa hao wameshindwa kupata wadhamini wenye mali isiyopungua thamani ya shilingi milioni 10 kila mmoja hatua ambayo imeamuriwa kupelekwa mahabusu hadi Machi 23, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.