**********************
NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Mwanza,limewaasa na kuwataka wanasiasa nchini kufanya siasa za ustaarabu zenye tija, wakitanguliza maslahi ya nchi badala ya maslahi binafsi.
Pia limempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa usikivu,ikiwemo Mahakama na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP),Sylvester Mwakitalu,kumfutia mashitaka ya tuhuma za ugaidi,Mwenyekiti wa CHADEMA,Freeman Mbowe na wenzake wakiwemo walokuwa wakikabiliwa na tuhuma za aina hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana kwa waandishi wa habari na Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke kuhusu kuachiwa kwa Mbowe pamoja na watuhumiwa wengine wa ugaidi nchini lakini pia kuelekea mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu.
Alisema Mbowe kuachiwa huru ni jambo jema la kufurahisha,limeleta maelewano na utangamano miongoni mwa Watanzania ambao awali walitenganishwa na kadhia hiyo baadhi wakishinda mahakamani na kwenye luninga kufutilia matokeo ya kesi hiyo.
Sheikhe Kabeke alisema Watanzania wanatamani kuona wanasiasa wakifanya siasa za ustaarabu,kiungwana, utu na kuheshimiana,siasa za kuweka mbele maslahi ya nchi na si maslahi binafsi.
“Kwa ujumla suala la Mbowe na watuhumiwa wengine limeisha vizuri,lituache tukiwa wamoja kama nchi na taifa bila kujali itikadi za vyama vya siasa na dini zetu,kama Watanzania tunao wajibu wa kuendeleza utulivu tukijenga nchi na kuchapa kazi kama alivyokaririwa Mbowe akimwambia Rais Samia kuwa sasa tujenge nchi,tusaidiane kujenga nchi yetu,”alisema.
Sheikhe huyo wa mkoa alidai kesi ya Mbowe ilisababisha mgogoro na maneno ya kuvutana na kusigana,DDP kuiondoa baada ya kuona hana nia ya kuendelea nayo licha ya mahakama kumwona ana kesi ya kujibu,hivyo wapenda haki na amani wanaotaka kutimiza wajibu wao ni muda wa kutulia na kuendelea kuchapa kazi.
Alisema BAKWATA ilikuwa na shida kubwa kupitia kwenye mabaraza yao na kwa Mufti Mkuu,Sheikhe Abubakar Zuber Bin Ali Mbwana,waliiomba sana serikali ifanye uchunguzi wa kutosha dhidi ya watu waliokuwa mahabusu kwa tuhuma za ugaidi.
Kwamba, ambao ingethibitika kuhusika kwa namna moja ama nyingine wachukuliwe hatua na wasiokuwa na hatia,waachiwe waendelee na uhuru wao.
“Ndani ya wiki mbili au tatu si Mwanza tu,Arusha,Dar es Salaam na Tanzania nzima, wananchi wameshuhudia na kusikia,kwa niaba ya BAKWATA nitumie nafasi hii kumpongeza kwa dhati mwendesha mashitaka mkuu wa serikali kwa busara na hekima aliyotumia kuwaachia watuhumiwa kwa kutokuwa na nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yao,” alisema Sheikhe Kabeke.
Pia alimshukuru kwa jambo ambalo hapa nchini lilikuwa tatizo,kwa kulitazama lilikuwa na shida nalo ni suala la kiongozi wa chama kikuu cha upinzani (CHADEMA) tangu akamatwe Julai 2021 pamoja na wenzake kesi yake iliendelea mahakamani na haikuwa kificho.
Alisema zilifanywa jitihada kwa wanasiasa na watu mbalimbali na utaona kadhia hiyo haikuwa na taswira nzuri lakini hatimaye viongozi wa dini wakiwa kwenye mazungumzo na Rais Samia walimwambia busara na hekima itumike kwenye kesi ya Mbowe na wenzake.
Sheikhe Kabeke alisema Mufti Sheikhe Mkuu wa Tanzania,Abubakar Zuberi Mbwana,ni miongoni mwa waliowasilisha hoja hiyo, hivyo DDP kwa nafasi yake aliiomba mahakama kuiondoa kesi hiyo ikaridhia.
“Hapa naipongeza Mahakama kwa kukubali ombi la DPP, pia Rais Samia kwa usikivu wake,na hapa niliweke vizuri isionekane anaingilia mihimili mingine (mahakama na bunge),mihimili yote mitatu,Serikali,Bunge na Mahakama,Mh.Rais ni Amiri Jeshi Mkuu wa vyombo vya ulinzi na usalama,”
“Ndiye kiongozi mkuu wa nchi,kubwa tunampongeza kwa usikivu wake,maana kwenye hilo jambo katika mkutano wa vyama vya siasa Mh.Zitto Kabwe alilizungumza,” alisema Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Mwanza.
Aliongeza kuwa Rais Samia alipokwenda Ubelgiji,Tundu Lissu alilizungumza na utaona ni kiongozi wa aina gani hata Machi 4, baada ya Mbowe kuachiwa alimkaribisha Ikulu kwa mazungumzo,ni jambo linalotia moyo na kuifanya nchi yetu kuwa amani na utulivu.
“Kwa lugha nzuri na nyepesi BAKWATA inampongeza sana Rais Samia,pia Mufti na viongozi wote wa dini kwa namna walivyoshirikiana kuhakikisha busara na hekima inatumika hatimaye Mbowe kuachiwa huru na kuungana na familia yake,”alisema.
Wakati huohuo Sheikhe Kabeke amesema Rais Samia anapotimiza mwaka mmoja Ikulu baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania,John Pombe Magufuli,yapo mengi ya kujivunia kwenye maendeleo.
Mwenyekiti Mwenza huyo wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Mwanza alisema licha ya kifo cha Magufuli nchi imeendelea kuwa imara na salama, hivyo Watanzania waendelee kuomba sababu jambo hilo lilitokea kwa mpango na mapenzi ya Mungu.
“Kimsingi tumeona Rais Mama Samia, Machi 19,mwaka huu, anatimiza mwaka mmoja madarakani,ameweza kuvaa viatu vile na ana fit,tumeona kazi anayofanya ni ya aina yake,tuliona alivyomaliza mgororo na Kenya baada ya mahindi yetu kuzuiwa,ukiyachukua hayo ni Rais wa mfano,”alisema.
Sheikhe huyo wa mkoa alisema nchi inaendelea kuimarika,kuna utulivu, amani na usalama,makusanyo ya kodi yameongezeka, amefanya ziara nchi za Ulaya zinazotuunga mkono kwenye maendeleo,amekwenda Dubai kushawishi wawekezaji, amejishusha na kurekodi filamu ya Royal Tour kuhamasisha utalii duniani.
Pia ameiheshimisha nchi kimataifa kuwa ni Taifa huru linaloendelea na ukombozi wa kiuchumi kupitia miradi ya kimkakati inayojengwa kote nchini,ameendelea kuwa mtetezi wa bodaboda,wajasiriamali wadogo kuhakikisha wanaheshimiwa na serikali yake inalinda shughuli zao bila kubughudhiwa na mamlaka za umma ikiwemo TRA na vyombo vya usalama.
Aidha Rais Samia ameimarisha mazingira ya uwekezaji nchini ambapo wawekezaji wamekiri hadharani kuwepo tofauti ya maboresho ya kibiashara huku mwekezaji Dangote wa kiwanda kikubwa cha saruji nchini, ameridhishwa na mazingira ya sasa kuwa hayana urasimu na milango ya biashara imefunguka na yupo tayari kuongeza uwekezaji wa kiwanda kingine kikubwa.
“Mh.Rais Samia aliilekeza TRA kufungua akaunti za wafanyabiashara zilizofungwa kwa sababu mbalimbali na wakae mezani kuona namna bora ya kutatua changamoto iliyosababisha zifungwe,hilo limetekelezwa,”alisema.
Sheikhe huyo wa Mkoa wa Mwanza alimshukuru Rais kwa kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, watuhumiwa wa vitendo hivyo wamewekwa pembeni uchunguzi ufanyike ikiwemo huko bandarini na hazina.
Kwa mujibu wa Sheikhe Kabeke Rais Samia ameendeleza ujenzi wa miradi ya kimkakati ya reli ya SGR, Bwawa la Nyerere na Daraja la J P Magufuli kwa kasi ya ajabu ikiwa ni kuenzi kwa vitendo kazi na maono ya mtangulizi wake picha isiyo na shaka ya kuwa kitu kimoja.
“Ukiachilia hayo kasi ya kukuza na kufanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania imeongezek, ulinzi na usalama ndani na nje ya mipaka umeirika,amepambana vikali na madawa ya kulevya,mauaji ya maalbino hayapo,matukio ya wizi na ujambazi yamepungua baada kutaka kumjaribu ,”alisema kiongozi huyo wa dini.
Ilani ya uchaguzi 2020 – 2025 inatekelezwa vyema kwa vitendo,shughuli za serikali zinafanyika bila mkwamo wowote ule.