WAFANYABIASHARA wa Soko la Kimataifa la Samaki,Kirumba mkoani Mwanza,wamelalamikia utitiri wa tozo,ushuru wa mazao ya samaki na vibali vya usafirishaji kuwa umesababisha kudorora kwa biashara kwenye soko hilo.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa soko hilo, Erasto Barusha aliieleza Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi,Kifua Kikuu,Dawa za kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza kuwa wanatozwa ushuru mkubwa na tozo mbalimbali zinazosababisha walimbikie soko hilo.
Alisema tozo na ushuru wanaotozwa umesababisha soko hilo kudorora,watu kukosa kazi na baadhi ya wanawake kujiingiza kwenye biashara ya ngono kupata fedha za kujikimu na wengine kujikuta wakiambukizwa Ukimwi na magonjwa yanayotokana na ngono.
“Utiriri wa kodi, masoko ya dagaa yapo matatu Kanda ya Ziwa,leseni na vibali vya kusafirishia mzigo vinagongwa mhuri na halmashauri lakini inakamatwa njiani sababu TRA imeweka vikwazo,bunge linapotunga sheria liangalie,”alisema Barusha.
Pia Mwenyekiti huyo wa Wafanyabiashara alisema Ziwa Victoria siku zijazo litabaki tupu,samaki wanazidi kupungua sababu ya uvuvi haramu na uvuvi usio na muda maalum lakini baadhi ya wavuvi wamepata elimu ya kutosha ya ufugaji wa samaki ili watumie fursa ya uchumi wa bluu na kushauri Bunge litunge sheria maalumu ili kudhibiti uvuvi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko hilo la Kimataifa la Samaki Kirumba, Fikiri Magafu,alisema wageni wanatoka nchi jirani na baadhi ya Watanzania na kwenda visiwani kununua samaki kunawanyima fursa wafanyabiashara wa soko hilo.
“Utaratibu wa vibali vya kusafirisha samaki unachangia vitendo vya rushwa sababu vinatolewa na binadamu,vitolewe eneo moja na kazi hiyo ifanywe na maofisa wa halmashauri Watanzania wapate huduma,”alisema.
“Masoko ya samaki yalijengwa yawanufaishe wavuvi na wafanyabiashara,lakini wananchi wasio waaminifu wanawapeleka wageni visiwani,wenye mitaji midogo hatuwezi kufanya biashara tena,”alisema.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega,alisema serikali kupitia wizara yenye dhamana ya sekta ya uvuvi inafuatilia kudorora kwa biashara soko la Kirumba ili kufahamu tatizo ni nini.
“Lengo ni kuona biashara hiyo inapamba moto sababu ina mchango mkubwa wa pato la taifa.Zipo hoja hapa zinagusa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pia Serikali za Mitaa (TAMISEMI)kuhusu tozo za mazao ya samaki,yawezekana zipo zinazotozwa hazipo kisheria bali kwa matamko,tukikaa pamoja na kuzipitia tutapata muafaka,”alisema.
Ulega alisema hoja ya ushuru na mrabaha wa mazao ya samaki yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi,ilishazungumzwa na Waziri (Mashimba Ndaki),hivyo wanaopeleka nje wataendelea kutozwa asilimia 0.16.
Pia kusitishwa kwa ushuru wa samaki kwa wafanyabiashara wasiosafirisha nje kunalenga kutafuta tiba ya kudumu ili kutomwumiza asiyesafirisha nje,na yawezekana wanapeleka kwa kutumia udhaifu wa mipaka na kuikosesha serikali mapato.
Naibu Waziri huyo wa Uvuvi alionya mfanyabiashara asiyepeleka samaki nje asibughudhiwe,aachwe afanye biashara na wageni kutoka nchi jirani kwenda visiwani moja kwa moja,kununua mazao ya samaki,kunasbabisha serikali kupata tabu ya kudhibiti shughuli haramu za uvuvi.
“Tumejipanga katika usimamizi wa sheria,wageni wanaotoka nje ya nchi hawataruhusiwa kukunua samaki popote isipokuwa kwenye masoko yaliyojengwa kwa biashara hiyo ili kuondoa uholela huo,hii itasaidia na tutafanya mabadiliko kwenye kanuni halmashauri zote zifuate msimamo huo wa Wizara ya Uvuvi,”alsema Ulega.
Aidha vibali vya usafirishaji wa samaki kutolewa pamoja,alieleza kuwa kodi ilikuwa haikusanyi lakini maofisa uvuvi wachache wanaruhusiwa kutoa vibali vya ndani ya wilaya na mkoa,ili kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali.