Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrance Mafuru akikata utepe kuzindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), iliyozinduliwa jijini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB Bw. Godfred Mbanyi, na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Jacob Kibona.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrance Mafuru (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) Bw. Jacob Kibona, wakionesha mpango kazi uliozinduliwa wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya (PSPTB), jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrance Mafuru (wa pili kulia) akimkabidhi mpangokazi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Bw. Jacob Kibona, baada ya kuzinduliwa kwa bodi hiyo jijini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB Bw. Godfred Mbanyi, na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma wa PSPTB Bi. Shamim Mdee.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrance Mafuru akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), jijini Dodoma
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Bw. Jacob Kibona, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Bw. Godfred Mbanyi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi hiyo, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrance (katikati walioketi) Mafuru akiwa katika picha ya Pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), mara baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Dodoma.
Menejimenti ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), na wageni waalikwa wakifuatilia shughuli ya uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya PSPTB, iliyozinduliwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrance Mafuru (hayumo pichani), jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Bw. Jacob Kibona, akimkabidhi mpango kazi mmoja wa wajumbe wa Bodi hiyo Bi. Esther Manyesha, mara baada ya kuzinduliwa kwa Bodi hiyo. Wa pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrance Mafuru, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Bw. Godfred Mbanyi na wa pili kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma wa Bodi hiyo Bi. Shamim Mdee.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)
********************
Na. Saidina Msangi, WFM- Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), kuchukua hatua za kinidhamu kwa wanaokiuka maadili ya taaluma ya ununuzi na ugavi.
Maagizo hayo yalitolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrance Mafuru kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya PSPTB, jijini Dodoma.
Alisema kuwa Bodi hiyo ina jukumu la kusimamia maadili na mienendo ya Wataalam ikiwa ni pamoja na uhuishwaji na utengenezwaji wa mitaala inayozingatia umahili wa kitaaluma na mahitaji ya soko, uandaaji na usimamiaji wa miongozo mbalimbali inayohusu taaluma hiyo.
“Wadau wa ununuzi na ugavi wana matumaini makubwa kutoka kwenu kwani nyie ndio mtatoa dira chanya katika kutekeleza majukumu yao, mkasimamie tafiti mbalimbali zinazohusu taaluma na kutoa majibu kwa changamoto zinazojitokeza kwenye taaluma ili kuongeza tija katika utendaji,” alisema Bw. Mafuru.
Alisisitiza kuwa Bodi hiyo ina wajibu wa kusimamia utoaji wa mafunzo endelevu kwa wataalam na wadau wengine kwenye mnyororo wa ununuzi na ugavi, kufanya kazi za ushauri zinazohusu taaluma ya ununuzi na ugavi na kusimamia vyema matumizi ya tehama na mifumo ya kielectroniki katika shughuli za kusajili wataalam.
Aidha, Bw. Mafuru aliihakikishia Bodi hiyo kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itaendeleza ushirikiano na Bodi ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa hatua zinazolenga kuondoa kabisa uzembe na ukiukwaji wa maadili katika fani ya ununuzi na ugavi kwani pesa nyingi za Serikali, zinatumika kupitia taaluma hiyo.
Alitoa rai kwa waajiri nchini kutoa ushirikiano kwa Bodi hiyo, hususani usimamizi wa maadili kwa wataalam waliosajiliwa na Bodi kwa kutoa taarifa kwenye Bodi zinazohusiana na ukiukwaji wa maadili kwa wataalam, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwani hakuna ufanisi bila maadili na weledi.
“Hakikisheni waajiri wote wanaajiri watumishi wenye sifa stahiki zinazotambuliwa na sheria ya PSPTB na kuzingatia mahitaji yaliyopo kwenye Waraka wa Maendeleo ya Utumishi Na. 3 wa mwaka 2015 wa kada zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango”, alisisitiza Bw. Mafuru.
Bw. Mafuru alimpongeza Mwenyekiti na wajumbe wa Bodi Bw. Jacob Kibona, kwa kuteuliwa na kuaminiwa kuisimamia Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Novemba 2021 hadi Novemba 2024.
Pia alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Ndugu Godfred Mbanyi kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mtendaji Mkuu wa PSPTB.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PSPTB Bw. Jacob Kibona, aliahidi kuwa Bodi itasimamia na kuimarisha taaluma ya ununuzi na ugavi sambamba na kuongeza nguvu ya kupambana na vitendo vyote vinavyokinzana na maadili ya kitaaluma ikiwemo ubadhilifu wa mali, rushwa na ukiukwaji wa taratibu za ununuzi na gavi.
Alisema kupitia Bodi hiyo itasimamia fedha zitakazotolewa na Serikali kwa ajili ya kukwamua shughuli zilizokwama kutokana na ukosefu wa fedha uliochangiwa na kutokuwa na bodi kwa muda mrefu na kuahidi kuisaidia Serikali kutekeleza malengo yake kwa weledi na kutoa huduma bora kwa Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Godfred Mbanyi alisema kuwa Menejimenti ya taasisi hiyo itatoa ushirikiano kwa Bodi hiyo na kuahidi kuwa watafanya kazi kwa weledi na kuwa itapokea ushauri na maelekezo ili kuongeza ufanisi.