Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Rainer Lukala (aliyevaa kofia) akiwasili katika shule ya sekondari Sintali wilaya ya Nkasi kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa matatu . Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (aliyevaa suti) na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Rainer Lukala (aliyevaa kofia) akiwa na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa leo wakati walipokagua mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Kasu ikiwa ni ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani katika wilaya ya Nkasi leo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Rainer Lukala akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo katika kijiji cha Sintali wilaya ya Nkasi ambapo ametoa wito kwa watumishi wa umma kusimamia miradi ili ikamilike kwa wakati
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Dkt. Benjamin Chota (kulia) akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Rukwa wakati walipotembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Kasu wilaya ya Nkasi leo.
********************
Na. OMM Rukwa
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Rukwa imeanza ziara ya siku saba ya ukaguzi wa utekelezaji Ilani ambapo katika siku ya kwanza imewataka watumishi wa umma kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati na ubora.
Kauli hiyo imetolewa leo (09 Machi, 2022) na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Rainer Lukala wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Sintali wilaya ya Nkasi mara baada ya kutembelea miradi ya maji, barabara na elimu.
Lukala alisema katika ziara hiyo wamebaini kati ya miradi minne waliyoikagua mitatu haijakamilika kwa wakati huku serikali imekwisha toa fedha kwa miradi husika hatua inayopelekea kero kwa wananchi.
“Kama chama tumewataka watumishi ambao ni waajiliwa wa serikali ya CCM watumie elimu yao kufanya kazi kwa bidii ili kero za wananchi kuhusu miradi kutokamilika kwa wakati iishe” alisema Lukala
Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa akiwa na Kamati ya Siasa Mkoa huo walikagua ujenzi wa kituo cha Afya Kasu ambapo taarifa ya wilaya ya Nkasi ilionesha kuwa shilingi Milioni 393.2 zimetumika kwenye majengo matatu ya wagonjwa wa nje, wodi ya wazazi na maabara kati ya shilingi Milioni 500 zilizotolewa na serikali mwaka 2021.
Lukala aliongeza kusema CCM inataka kuona miradi inakamilika katika kipindi kilichopangwa ili wananchi wanufaike ambapo alitoa wito kwa halmashauri ya Nkasi kuhakikisha mradi wa ujenzi kituo cha Afya Kasu unakamilika mwisho mwa mwezi Machi mwaka huu.
Nae Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Dkt. Benjamin Chota alisema kukamilika kwa kituo cha Afya Kasu kutawezesha wananchi 39,659 wa kata za Kasu na Chala kupata huduma za afya karibu zaidi.
Viongozi hao wa Chama Tawala walikagua pia mradi wa barabara ya Sintali –Nkana – Kala yenye urefu wa kilometa 65.1 ambayo ujenzi wake ulianza Septemba 2021 na itagharimu shilingi Milioni 576.5 zilizotolewa na serikali na ujenzi wake umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika Machi mwaka huu.
Mradi wa tatu uliokaguliwa ni ule wa maji katika kijiji cha Sintali ambao umegharimu shilingi Milioni 230 na umefikia asilimia 90 lakini bado vituo 12 vya kuchotea maji havijakamilika ambapo Mwenyekiti wa Kijiji cha hicho Linus Nyaoza alidai ulipaswa kukamilika mwezi Agosti mwaka jana.
Mradi wa nne uliokaguliwa na viongozi hao wa CCM Rukwa ni ule wa ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya sekondari Sintali ambayo yamekamilika na kugharimu shilingi Milioni 60 kupitia Mpango wa maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano ya UVIKO-19.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, hivi sasa tumeona jitihada zake za kutafuta fedha za miradi ya maendeleo hivyo lazima watumishi wasimamie miradi kwa ubora na kuzingatia thamani ya fedha” alisisitiza Lukala.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti anayeshiriki kwenye ziara hiyo aliwapongeza viongozi hao wa CCM kwa kupanga ziara hiyo kukagua shughuli za maendeleo kwenye halmashauri nne za mkoa wa Rukwa.
Mkirikiti alisema maelekezo yote yatafanyiwa kazi ili malengo ya Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya 2020- 2025 yaweze kutimia kwa kuondoa kero na kuchochea maendeleo ya wananchi.
Kamati hiyo ya Siasa ya Mkoa Kesho inaendelea na ziara yake katika Halmashauri ya Nkasi ambapo viongozi wa serikali wanaongozwa na Mkuu wa Mkoa Joseph Mkirikiti pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijualikali.