************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WANAWAKE wafanyakazi wa Benki ya NMB Tawi la Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, katika kusherehekea siku ya wanawake duniani, wamekabidhi makasha matano ya kuhifadhia uchafu ili kutunza mazingira ya soko la Mirerani.
Meneja wa huduma kwa wateja benki ya NMB Tawi la Mirerani Bahati Philemon amesema wamesherehekea siku ya wanawake duniani kwa kutoa makasha hayo kwa lengo la kutunza mazingira.
Bahati amesema pia wametoa elimu ya fedha kwa wanawake hao juu ya kufungua akaunti kuhifadhi fedha benki, kupatiwa mikopo na kukata bima ya biashara zao.
Ofisa afya wa mji mdogo wa Mirerani, Jovin Rweyemamu amewataka wafanyabiashara na wajasiriamali wa soko hilo kuyatumia makasha hayo kwa lengo lililokusudiwa.
Rweyemamu amesema haitaingia akilini kuja kusikia badala ya kuweka uchafu kwenye makasha hayo, baadhi yao wakaweka bidhaa zao za kuuza.
“Haitapendeza kukuta mjasiriamali ameweka njegere badala ya kusafisha na kutunza uchafu uliotumika kila siku kwenye pembe ya soko,” amesema.
Mmoja kati ya wajasiriamali wa soko la Mirerani, Evaresta Laurence ameishukuru benki ya NMB kwa kuwapatia msaada huo wa makasha ya kuhifadhi uchafu.
Evaresta amesema wamepatiwa elimu ya fedha hivyo wapo tayari kufungua akaunti na kuachana na mtindo wa kuweka fedha kwenye vibubu.