Meneja wa benki ya NMB Kanda ya kaskazini, Dismas prosper akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo ya “UmeBima”uliofanyika katika soko la Samunge lililopo jijini Arusha leo.(Happy Lazaro)
Waendesha bodaboda mbalimbali wakisikiliza elimu iliyokuwa ikitolewa na benki hiyo kwenye uzinduzi huo jijini Arusha leo.
Afisa habari mahusiano na elimu kwa umma kutoka kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoani Arusha,Abubakari Monela akitoa elimu katika uzinduzi huo.
**********************
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Benki ya NMB imezindua kampeni ya bima ijulikanayo kama “Umebima” kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo (Machinga) ambayo hutoa fidia dhidi ya upotevu wa mali za biashara kutokana na moto au mafuriko sokoni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo jijini Arusha katika soko la Samunge ,Meneja wa benki ya NMB Kanda ya kaskazini,Dismas Prosper amesema kuwa,bima hiyo inawasaidia kuwekea kinga katika majanga ya moto na mafuriko wa mali zao ili kuhakikisha biashara zao zinakuwa salama dhidi ya majanga hayo.
Dismas amesema kuwa,bima hiyo inalenga zaidi wafanyabiashara wa masoko na wamachinga katika kuhakikisha bidhaa zao zinakuwa salama muda wote na pindi majanga yanapotokea wanaweza kufidiwa hasara waliyoipata.
Amesema kuwa, licha ya wananchi kuwa na uelewa juu ya maswala ya bima bado changamoto iliyopo ni kuwepo kwa mwitikio mdogo wa wananchi kujiunga na bima hiyo ,ndio maana benki hiyo imeamua kuja na kampeni hiyo ambayo itafanyika katika mikoa ya Arusha,Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
“Bima hii itakuwa inatolewa katika matawi yote ya benki ili kuhakikisha wafanyabiashara hao wanapata huduma hiyo kwa karibu na muda wowote ,hivyo nawaomba Sana kuchangamkia fursa hiyo ambayo ni muhimu na imeweza kuwanufaisha wengi waliokumbwa na majanga mbalimbali.”amesema .
Naye Afisa habari mahusiano na elimu kwa umma kutoka kikosi cha zimamoto na uokoaji ,Abubakari Monela akizungumza katika halfa hiyo amewataka wafanyabiashara hao kutumia fursa ya kukata bima hiyo kwani ina manufaa makubwa Sana kwao hususani wanapopatwa na majanga mbalimbali.
Monela amesema kuwa, jamii inapaswa kufahamu kuhusu bima hiyo kwani ina manufaa makubwa sana kwao, huku akiwataka kupiga simu ofisi za zimamoto mara moja pindi tu wanapokutana na mikasa ya moto ili kuweza kupata huduma za haraka kabla madhara hayajatokea makubwa.
Naye Mkuu wa soko la Samunge , Jeremiah Katemi amesema kuwa, wanashukuru Sana benki hiyo kwa kuja na kampeni hiyo ya bima ambayo inatoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kukata bima kwa ajili ya biashara zao na kuweza kuwa na uhakika wa bidhaa zao pindi wanapokumbana na majanga mbalimbali.
Katemi amewataka wafanyabiashara kukatia bima biashara zao kwani ina faida kubwa na imewasaidia wafanyabiashara wengi pindi wanapokumbana na majanga mbalimbali yakiwemo ya moto ,na mafuriko ambapo kinachofidiwa ni mali za biashara dhidi ya majanga ya moto na mafuriko.