Mhamasishaji Rika Senorita Frank akizungumza katika mafunzo hayo namna alivyonufaika na shirika hilo katika kupinga ukatili wa kijinsia .
Afisa mradi wa Binti na maendeleo (BIMA)kutoka shirika la DSW,Juliana Mndanga akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika ofisi za shirika hilo leo (Happy Lazaro).
************************
Happy Lazaro, Arusha
Arusha.Shirika la afya na maendeleo ya vijana DSW limetoa mafunzo kwa watekeleza sheria kutoka ngazi mbalimbali katika kuwajengea uwezo juu ya umuhimu wa utekelezaji kuhusu haki za msingi kwa wanawake na wanaume kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa utoaji wa mafunzo hayo Jijini Arusha leo,Afisa mradi wa binti na maendeleo (BIMA) uliopo chini ya shirika la DSW ,Juliana Mndanga amesema kuwa, lengo la kuwakutanisha wadau hao ni kuwakumbusha wajibu wao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kuweka mikakati ya namna ya kulinda haki za wanawake kwa maendeleo endelevu.
Amesema kuwa,wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wadau mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha ukatili wa kijinsia unakomeshwa katika ngazi mbalimbali kwani vitendo hivyo vimekuwa vikiendelea kufanyika kutoka na wengi wao kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya maswala hayo.
“Mafunzo haya leo tumewashirikisha polisi, walimu,wanafunzi,wawakilishi wa kata,mashirika binafsi,watendaji wa kata na vijiji pamoja na viongozi wa mkoa na halmashauri kwani wadau hao ndio walengwa wakubwa waliopo kwenye maeneo ambayo ukatili umekuwa ukifanyika kila wakati na wao ndio mabalozi watakaoenda kutoa elimu hiyo kwa jamii”amesema Juliana.
Amesema kuwa, wamekuwa wakitoa elimu juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia pamoja na kupinga ukeketaji kwa wasichana ambapo wengi wao wameweza kuzifahamu haki zao na kuendelea kupinga ukatili huo na kuwa mabalozi wa kuwaelimisha wengine juu ya kupinga ukatili huo.
Ameongeza kuwa, kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani inasema “kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu”ambapo jamii inapaswa kutambua kuwa kuna mipango mikakati na Sera zinazohakikisha haki sawa inapatikana huku akiwataka kutambua mikakati na Sera hizo katika kupinga ukatili katika jamii inayowazunguka.
Mkuu wa kitengo dawati la jinsia na watoto wilaya ya Arumeru,Salama Ally amesema kuwa, wamekuwa wakipokea ripoti mbalimbali za matukio ya kijinsia ikiwemo ubakaji,ulawiti,kudhalilishwa kingono maofisini ambapo wamekuwa wakishirikiana na shirika hilo kuhakikisha wanakomesha matukio hayo kwa kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka na kuweza kukomesha matukio hayo.
Salama amesema kuwa, wamekuwa wakitoa elimu kwa wanafunzi waliopo mashuleni kwani wamekuwa wakikutana na matukio ya ukatili ikiwemo kufanyiwa shambulio la aibu ambapo wanafunzi wengi wameweza kuwa mabalozi wa kutoa elimu hiyo kwa wengine baada ya kuwezeshwa .
Nao Wahamasishaji Rika waliowezeshwa na shirika hilo na kuweza kuwasaidia wengine,Senorita Frank na Amani Samweli wamesema kuwa, wameweza kuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu kwa wenzao mashuleni juu ya ukatili wa kijinsia ambao wamekuwa wakifanyiwa na wazazi wao pamoja na jamii yao hususani katika maswala ya ukeketaji kutokana na mila na desturi za jamii ya kimasai.
Wamesema kuwa,baada ya elimu hiyo wameweza kuanzisha klabu za kupinga ukatili wa kijinsia mashuleni ambapo wameweza kuokoa watoto sita ambao walikuwa wafanyiwe ukeketaji ,hivyo wanaendelea kutoa elimu zaidi katika kuhakikisha swala zima la ukatili wa kijinsia kwa wanawake linatokomezwa kabisa.