Afisa Mwandamizi wa Bima za mali na Ajali Bi.Erica Gabriel akielezea umuhimu wa kujiunga na Bima kwa wafanyabiashara wa soko la Karume Jijini Dar es Salaam Baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Karume wakiwasikiliza watumishi wa shirika la Bima la Taifa la NIC wakati wakiwapatia elimu ya Bima mara baada ya kuwatembelea eneo hilo leo tarehe 08/03/2022 kwaajili ya kuwapatia elimu.Baadhi ya watumishi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) wakiwa katika eneo la soko la Karume kwaajili ya kuwapatia elimu ya Bima wafanyabiashara wa soko hilo Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilala Kota Bw.Amini Migomba akizungumza mara baada ya Shirika la Bima kufika katika eneo la soko la Karume kwaajili ya kuwapatia elimu ya Bima wafanyabiashara wa soko hilo
********************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KATIKA kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Shirika la Bima la Taifa limewatembelea wanawake wa soko la Karume kwaajili ya kuwapatia elimu ya Bima ili kuondokana na hasara zitokanazo na majanga ya moto.
Akizungumza katika zoezi la utoaji elimu hiyo Meneja Rasilimali Watu, Bi.Veneranda Mpaze amesema kuwa kwa kutambua na kuthamini mchango wa Wanawake wameamua kukutana na wanawake wafanyabiashara wa soko la karume kwa kuwapa pole na kuwatia moyo waendelee na biashara zao.
Amesema NIC wanaamini katika usawa wa jinsia leo ni chachu ya maendeleo ya kesho ndiyo maana wapo kwaajili ya kuwapatia elimu ya bima na faida zake katika biashara.
“Katika Maadhimisho haya NIC natumia fursa hii kuwataarifu kwamba mnaweza kulinda biashara zenu na kuondokana na hasara za namna hii mkiwa na bima ya biashara kutoka NIC kwasababu utafidiwa kwa kurejeshewa kilichopotea endapo majanga kama haya yanatokea”. Amesema Bi.Veneranda.
Aidha amesema unaweza ukakata bima ya biashara yako kuanzia mtaji wa shilingi 25,000 mpaka shilingi milioni 18 utalipia shilingi 59,000 na VAT ndani yake.
Ameeleza kuwa kutokana na janga hili la moto, anawasihi wanawake kuchamkia bidhaa za LINDA MJENGO ambayo inampa Mtanzania kinga dhidi ya janga la moto kwenye nyumba yake.
“Kupitia Bima hii mteja akipata janga la moto, tetemeko au mafuriko, NIC itampatia asilimia 40% ya pesa yake ndani ya siku moja ili aweze kupata makazi mbadala wakati akijiandaa kujenga nyumba nyingine kwa pesa atakayolipwa na NIC”. Ameeleza
Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko Karume Bw.Geofrey Milonge amewapongeza NIC kuonesha moyo wa kuwajari kwa kuhakikisha wafanyabiashara wa eneo hilo wanafahamu umuhimu na faida ya kujiunga na Bima ya NIC.
Nae Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilala Kota Bw.Amini Migomba amesema NIC wameona umuhimu wao na kuona ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia wafanyabiashara wa soko hilo.
Amesema kupitia elimu hiyo wanayoitoa NIC kuhusu umuhimu wa Bima utasaidia wafanyabiashara wengi kujiunga na bima hiyo na kuondokana mfumo wa mwanzo wa kulialia kwa kukosa msaada.