***********************
NA FARIDA SAID MOROGORO.
Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mjini Morogoro kitengo cha Ufundi, wamekabidhiwa vitendea kazi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Milion 180,ili kukabiliana na upotevu wa maji, ambapo asilimia 39 ya maji yanayozalishwa hupotea bila kuwafikia walengwa na kusababisha hasara ya shilingi Milion 500 kwa kila mwezi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vitendea kazi hivyo ambavyo ni Pikipiki 30 na Gari moja Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mjini Morogoro Mhandisi Tamimu Katakweba amesema kupatikana kwa vitendea kazi hivyo kutarahisisha utendaji kazi wa mafundi wa mamlaka hiyo kuweza kufika kwa wakati eneo la tukio pindi taarifa ya upotevu wa maji itakaporipotiwa.
Amesema kuwa uzalishaji wa maji kwa mji wa Morogoro ni wastani wa Lita za ujazo 34,000 kwa siku huku mahitaji kwa siku yakiwa ni Lita za Ujazo 67,000 hivyo kufanya upungufu kufikia Lita za ujazo 33,000.
Aidha ameongeza kuwa Pamoja na upungufu huo bado asilimia 39 ya maji yanayozalishwa hupotea bila kuwafikia walengwa huku chanzo cha upotevu wa maji kikiwa ni uchakavu wa Miundombinu sambamba na Uharibifu unaofanywa na baadhi ya watu hasa wanaoendesha shughuli za kibinadamu kwenye maeneo hayo yaliyopitiwa na miundombinu
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi MORUWASA Prof.Romanus Ishengoma ameigiza Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mjini Morogoro kudhibiti upotevu wa maji ambayo husababishia mamlaka hasara kubwa kila mwezi, huku akisisitiza utunzaji na usimamizi mnzuri wa vifaa hivyo ili viweze kufanya kazi iliyokusudiwa na sio kufanya shughili nyingine.
Nae Meneja EWURA kanda ya Mashariki Nyirabu Musira ameipongeza MURUWASA kwa hatua walioifikia ya ununzi ununuzi wa vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia katika utendaji wao wa kazi za kila siku kwa ufanisi wa hali ya juu.