Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,akizungumza wanafunzi wa shule ya Sekondari Benjamin Mkapa na shule za jirani (hawapo pichani) mara baada ya kufanya ziara maalum katika shule hiyo leo March 7,2022 jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa.
WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Benjamin Mkapa na shule za jirani wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) wakati akizungumza nao mara baada ya kufanya ziara maalum katika shule hiyo leo March 7,2022 jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………….
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema serikali inatambua changamoto zinawakabili watoto wenye mahitaji maalum nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika shule ya sekondari Benjamin Mkapa alipofanya ziara maalum katika shule hiyo kuzungumza na wanafunzi wa shule hiyo na shule za jirani Mhe. Rais amesema kutokana na hilo serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuna mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia ili kuwezesha watoto hao wananufaika na fursa za elimu kwa manufaa binafsi na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Rais ameongeza kuwa katika kukabiliana na changanoto hiyo, serikali imeendelea kutekeleza Mkakati wa Tatu wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi katika ngazi zote za elimu kuanzia elimu ya awali mpaka elimu ya juu ikuwemo vyuo vya ufundi, ualimu na Maendeleo ya Jamii uliotolewa na Wizara ya Elimu.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa mkakati huo unalenga kutoa fursa za upatikanaji wa elimu jumuishi iliyo bora kwa watu wote ili kujenga jamii jumuishi na kuwa na mfumo wa elimu unaotoa fursa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kupata elimu bila vikwazo vya kimtazamo, kimanzingira, kiuchumi na kitaasisi katika ngazi zote.
Ameendelea kueleza kuwa pamoja na Mkakati huo, serikali pia imetoa mwongozo kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa elimu maalum na jumuishi nchini ambapo ametaja miongozo hiyo kuwa ni Mwongozo wa Usimamizi wa Uendeshaji wa taasisi zinazotoa elimu maalum na jumuishi na Mwongozo wa Chakula Shuleni wa Mwaka 2021.
Akitoa salam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema katika kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata fursa za masomo tayari wizara imeshakamilisha ujenzi wa shule maalum ya msingi mpya Lukuledi iliyopo Masasi na Shule ya Sekondari Maalum Patandi iliyoko Mkoani Arusha ambazo tayari zimeshaanza kuchukua wanafunzi.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa mwaka huu pia vitabu 93,366 vya wanafunzi wenye uoni hafifu na wasioona vimechapishwa na kusambazwa katika shule, viti mwendo 1, 334 vimenunuliwa kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu pamoja na vishikwambi (tablets) kwa ajili ya shule 15 za msingi zinazochukua wanafunzi viziwi.
Aidha, Prof. Mkenda amewataka wazazi na walezi wenye mahitaji maalum kuhakikisha wanawapeleka shule watoto wenye mahitaji maalum ili kuwapa nafasi kutumia fursa ambayo serikali imewekeza kwa ajili yao.
Naye Mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Emmanuel Mzena amemshukuru rais kwa kufika shuleni hapo na kwa serikali yake kuwekeza zaidi katika kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum kama yeye wanasoma katika mazingira rafiki.