Mratibu wa TASAF Jiji la Dodoma, Sekunda Kasese akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake
*****************
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANAWAKE katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa kufanya kazi kwa bidii na mshikamano ili kuhakikisha jiji hilo linasonga mbele katika nyanja zote za maendeleo.
Ushauri huo ulitolewa na Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sekunda Kasese katika mahojiano maalum na Dodoma City TV ofisini kwake mwishoni mwa mwiki hii.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwashauri wanawake katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufanya kufanya kazi kwa bidii, weledi, maarifa na mshikamano ili kuhakikisha jiji letu linasonga mbele katika nyanja zote za maendeleo” alisema Mratibu Kasese.
Akiongelea kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mwaka 2022 isemayo “Kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu; tujitokeze kuhesabiwa” aliitaja kuwa ni muhimu. Kaulimbiu hiyo ni muhimu sana kushirikisha jinsia zote katika mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya jamii na taifa kwa ujumla, aliongeza.
“Wanawake ni kundi kubwa sana katika jamii na wao wakishirikishwa katika mipango ya maendeleo, wanawake wanaweza na wanafanya vizuri. Hivyo, wakijitokeza kuhesabiwa kwa sababu ni sehemu kubwa ya jamii yetu wataiwezesha serikali kufikia malengo yake” alisema Mratibu Kasese.
Kuhusu mpango wa kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, alisema kuwa unafanya vizuri.
“Mpango wa kunusuru kaya masikini unafanya vizuri na unaendelea kufanya vizuri katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuinua hali ya umasikini wa jamii. Kundi kubwa la walengwa walio katika mpango wa kunusuru kaya masikini ni wanawake. Katika Jiji la Dodoma tunajumla ya wanufaika 26,289, kati ya hao 16,101 ni wanawake walio katika rika mbalimbali na 10,188 ni wanaume. Wengi wanaopokea ruzuku ni wanawake.
Tunajua mwanamke akipokea ruzuku ni fedha inayomsaidia yeye pamoja na kaya kwa ujumla sababu anapochukua fedha hiyo haipeleki katika mambo mengine yasiyofaa mfano ulevi wa kupindukia. Fedha anayopata anaipeleka kwenye biashara ndogondogo na shughuli nyingine za uzalishaji mali ili kuongeza kipato cha kaya” alisisitiza Mratibu Kasese.
Mratibu huyo alisema kuwa wanawake wanufaika wa TASAF walio katika vikundi wanapata fursa ya mikopo ya wanawake ya asilimia nne kutoka mapato ya ndani inayotolewa na halmashauri ya jiji hilo. “Ni ukweli usifichika kuwa mikopo inayotolewa na halmashauri kutoka mapato ya ndani imewanufaisha wanawake wengi tu wanufaika wa TASAF” alisema.
Alisema kuwa wanawake hao wamekuwa wakinufaika na mafunzo ya ujasiriamali kupitia ‘community sessions’ ambazo wakufunzi mbalimbali hutoa elimu ya ujasiriamali, masuala ya lishe, ufugaji, utengenezaji sabuni na vyungu.
Maadhimishi ya siku ya wanawake duniani mwaka 2022 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kizazi cha haki na usawa kwa naendeleo endelevu, tujitokeze kuhesabiwa” na ngazi ya Mkoa wa Dodoma yatafanyika wilayani Chemba.