*************************
Adeladius Makwega-DODOMA
Wanyakyusa ni kabila linalopatikana Kusini Magharibi mwa Tanzania ya leo, awali ilikuwa ni sehemu ya Wilaya ya Rungwe huku baadaye ilikafahamika kama Tukuyu. Kwa mtazamo wa Lugha Wanyakyusa ni kabila linalowekwa katika kundi la wabantu.
Kabila hili limegawanyika katika makundi makubwa manne. Kwanza wale wanaoishi katika ukingo wa ziwa, wale wanaoishi eneo la Masoko hawa wanaoishi katika ya eneo la kati , wale wanaoishi mashariki na jirani na Milima wa Livingstone huko Selya na wapo wale wa Kaskazini Kukwe na Lugulu.
Ndani ya kabila hilo yapo makundi madogo madogo mno ambayo yanatumia lugha za zamani za kabila hilo mathalani WAPONJA hawa wanapatikana katika miinuko ya Kukwe, WANYIKA wakipatikana katika miinuko hiyo hiyo. Pia wapo WANDALI wanaopatikana katika miinuko ya upande wa magharibi. Pia wapo WALAMBYA na WAHENGA hawa wapo upande wa kusini magharibi wa eneo hilo.
Inaaminika kuwa Wanyakyusa walifika katika eneo hilo wakitokea MAHENGE-ULANGA MOROGORO kupitia milima ya Livingstone na wakaweka kambi katika eneo hilo la ukanda wa Rungwe, walipofika huko walizidi kuongezeka na kuendelea kuwa wengi kutokana na sifa yao kubwa ya namna wanavyoshirikiana na namna wanavyoishi wa pamoja wakishiriki shughuli za kilimo na ufugaji.
Mwanakwetu kama yupo Mnyakyusa aliyewahi kukutana na Mpogoro alafu akamfanyia vitimbwi basi ni vizuri akamuomba msamaha mapema kabla jua alijazama maana Mnyakyusa ni mtoto wa Mpogoro. Hilo mwanakwetu mimi nalitoa kama zawadi wa ndugu zangu Wanyakyusa.
Hali hii ilifanya hadi waweze kufika hadi Mbeya, katika Bonde la Usangu, Chunya, Songwe na hata Mbozi. Wakiwa katika eneo hilo makabila mengine yalishawishika kujifunza kinyakyusa ili kuweza kuwasiliana na ndugu hawa.
Eneo hili ambalo Wanyakyusa waliloweka kambi lilikuwa na ardhi nzuri yenye rutuba mno ambayo ipo katika ukanda wa bonde la Ufa likiwa chini ya urefu wafuti 10000 mpaka ukanda wa Wandali. Eneo hili linaishia katika upande wa juu wa Rungwe wenye udongo wa volkano katika milima ya Poroto kati ya futi 8000-10000.
Kwa bahati nzuri eneo hili linajaliwa kupata mvua kubwa sana kwa mwaka huku maji hayo yakitoka katika vilima na kushuka mabondeni wakati wa mismu wa mvua kubwa kubwa hasa mwezi Februari hadi Aprili ya kila mwaka. Ndiyo kusema ndiyo maana Wanyakyusa ni wajuzi wa kilimo bora na wafugaji bora wa mifugo.
Katikati ya karne ya 19 eneo la Maziwa Makuu ya Afrika ya Kati lilisumbuliwa mno na Wabemba, Wayao na Wangoni katika makundi kadhaa hasa hasa kwa Wasangu na Wahehe. Huku wakati huo Waarabu nao wakiwamo katika ukanda huo kwa misafara yao ya kibiashara.
Wanyakyusa walikuwa na desturi ya kutembea na silaha wakati wote, waliokuwa wakidhani ni wakati wa shida, silaha hizo kama vile mikuki na mishale. Kwa desturi Wanyakyusa hawakuingizwa katika biashara ya watumwa. Pia kabila hili hawakuwa na tabia ya kuacha ardhi yao yenye rutuba, walibakia katika maeneo hayo hayo wakifanya shughuli za kilimo na ufugaji.
Kwa bahati nzuri eneo lao halikupitiwa hata kidogo na njia za biashara za utumwa lakini hicho hakikuwa kisingizio cha waarabu kutolitamani eneo hilo. Inadaiwa kuwa Wanyakyusa walikuwa ni wapiganaji mahiri huku tamaa hiyo ya Waarabu kufika huko ikitishwa na uwezo wa Wanyakyusa vitani. Kwa hiyo Mwarabu hakufika huko.
Kwa kuwa walikuwa katika eneo lenye maji ya kutosha, vyakula vingi na huku mifugo yao ikinawili mno, tamaa ya wageni kufika huko iliongezeka mno.
Walipofika Wamisionari jirani na ukanda huo Chifu wa Wasangu Merere alidiriki kusema kuwa analimiki eneo la Kukwe. Jambo hilo halikuwa na ukweli wowote bali Chifu Merere miaka minne nyuma kabla ya kufika Wamisionari hao alipojaribu kulisogelea eneo hilo la Kukwe ambalo ni la Wanyakyusa alipigwa vilivyo. Wakati huo Wanyakyusa walikuwa wakiongozwa na Chifu wao aliyefahamika kama CHIFU MWAMAKULA. Inakadiliwa uvamizi wa Chifu Merere kwa Chifu Mwamakula ulikuwa mwaka 1892.
Wangoni wanasema kuwa kabla hawajafika ufipani waliwavamia Wanyakyusa mwaka 1840 na walipofika ufipani waligawanyika katika makundi makubwa mawili mara baada ya kufariki kiongozi wao aliyefahamika kama Zwangendaba.
Wangoni hao kulikuwa na kundi la watu wa Mbelwa ambao walikwenda kuweka makaazi yao huko Malawi, na kundi la watu wa Magwangwara ambao walikwenda kuweka makaazi yao huko Songea kusini mwa Tanzania.
Watu wa Mbelwa waliishi upande wa juu wa miinuko ya Rungwe, baada ya kuondoka huko Ufipani na wakajigawa na wale wa Songea. Makundi yote mawili yalijaribu kuwachokoza Wanyakyusa naye CHIFU MWAKALOBO wa Selya aliwafurusha mbio mbio wakatokomea mbali kabisa ndiyo chanzo cha Wangoni hao kwenda Songea na wengine kwenda Malawi
Mwanakwetu hao ndiyo Wanyakyusa.
Je kipi kitaendelea subiri matini ijayo.