********************
Na Farida Said, Morogoro.
Jeshi la polisi Mkoa wa Morogoro limewakamata raia 17 wa Ethiopia wakiwa katika gari aina ya Toyota Alphard wakielekea mkoani Mbeya baada ya dereva wa gari hilo kushindwa kusimama katika kizuizi cha Mikumi mkoani humo.
Hayo yamelezwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Fortunas Musilimu wakati akizungumza na waandishi wa habari Marchi 5 ambapo amesema jeshi hilo limewakamata raia hao Machi 4, 2022 eneo la Ruaha Mbuyuni baada ya dereva wa gari hilo kutiliwa shaka na polisi.
Hata hivyo kamanda huyo amesema pia jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 50 kwa tuhuma mbalimbali katika operesheni ya kupambana na uhalifu iliyoanza Februari 26, 2022.
“Operesheni hii ya kupambana na uhalifu, ilianza Februari 26 hadi Marchi 4 mwaka huu na tayari tumewakamata watuhumiwa 46 wakiwemo raia 17 wa Ethiopia na operesheni hii itakuwa endelevu na kuhakikisha wahalifu wanaacha uhalifu.”amesema Kamanda Musilimu.
Kamanda amesema katika operesheni hiyo imewatia nguvuni watuhumiwa 16 wanaojihusisha na kuuza na kusambaza bhangi ambapo viroba vinne vyenye jumla ya kilo 80 huku vijana 13 wakikamatwa kwa kujihusisha na wizi maeneo ya masoko na katika minada ya Kikundi, Sabasaba na soko la Mawenzi.