Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MANAIBU Mawaziri Ridhiwani Kikwete na Abdallah Ulega, wameiomba Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kurasimisha Bandari bubu zilizopo kwenye mkoa wa Pwani ambazo zinavusha bidhaa kwa kukwepa ushuru hali inayosababisha kuinyima Serikali mapato.
Wakizungumza Mjini Kibaha wakati wa kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) Manaibu Mawaziri hao ,Ridhiwani Kikwete ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi na Abdallah Ulega Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi walisema , baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakikwepa ushuru kupitia Bandari bubu hizo.
Ridhiwani alisema bidhaa nyingi zimekuwa zikitokea Zanzibar hazilipiwi ushuru kwani zimekuwa zikipitishwa kwenye Bandari hizo ambazo ziko kwenye Bahari ya Hindi maeneo ya Kitame na Saadani ambapo wavushaji hufanya nyakati za usiku.
Alisema , bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na bidhaa za madukani zimekuwa zikivushwa na kuingia mtaani na kusababisha Serikali kukosa mapato.
“Ifike wakati badala ya kila mara kulalamika juu ya Bandari hizo ni vema zikarasimishwa ili zitumike kisheria na mapato ambayo yanapotea yaweze kuingia serikalini,”alisema Ridhiwani
Naye Abdallah Ulega alisema kuwa endapo Bandari hizo zitarasimishwa pia itasaidia kutumia bahari na mazao yake wakiwemo samaki aina ya Kambakochi ambao wanaliingizia Taifa fedha za kigeni.
Ulega alieleza, Rais Samia Suluhu Hassan anahimiza kuhusu uchumi wa bluu ambao ndiyo inahitaji utumike vizuri kwani humo kuna rasilimali nyingi kama vile majongoo bahari.
Alisema kuwa Mkuranga kuna maeneo kama Kisiju ,mbali ya shughuli za utalii ,Bandari ikirasimishwa mapato yatakuwa mengi tofauti na sasa ,
Awali Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alisema kuwa ushauri huo utapelekwa sehemu husika ili ufanyiwe kazi .
Alisema ,Pwani ni moja ya mikoa yenye Bandari bubu nyingi, licha ya changamoto hiyo lakini anavishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kudhibiti hali hiyo.