Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara iliyo chini ya Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) na kuitaka kujifunza kujenga hoja ya kuwezesha upatikanaji wa fedha ili kuongeza kasi ya utekelezaji.
Aidha aliwaasa wakandarasi walioaminiwa waache kujisahau Bali waongeze kasi ya ujenzi kwenye miradi ya miundombinu ya barabara waliyokabidhiwa kuijenga.
Kunenge aliyasema hayo wakati wa kikao cha bodi ya Barabara ya mkoa wa Pwani ambacho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilayala zote, wakurugenzi na Wabunge.
Alisema , Serikali inaendelea kutoa fedha kuongeza miradi mipya ili kuboresha sekta ya miundombinu na mkoa umejidhatiti kushirikiana na TARURA na TANROADS kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa maslahi ya wananchi.
Vilevile Kunenge aliipongeza TARURA na TANROADS kusimamia pia ujenzi wa daraja la Mbuchi kwani linakwenda kuondoa kero kwa wananchi.
“Nashukuru kuwa na timu nzuri ya watendaji na wataalamu,wananirahisishia utendaji wa kazi yangu,”
“Taasisi zinatakiwa kujenga hoja juu ya nini kifanyike ili waweze kupatiwa fedha na kutekeleza miradi ambayo inakwenda kuondoa vikwazo kwa wananchi”
Akizungumzia upande wa Barabara alisema ili kuwe na sababu kwanini fedha zitolewe, TARURA wanatakiwa kujenga hoja kwani hakuna atakayekupa kitu bila kujua umuhimu wake na hiyo inasababishwa na kuwa na mahitaji mengi ya fedha kwenye miradi mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdallah Ulega alitaka barabara zenye viwango vya kupandishwa hadhi ziangaliwe kwa jicho la tatu ikiwemo ile ya Vikindu-Sangatini-Kigamboni.
Nae Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) mkoa wa Pwani Mhandisi, Leopold Runji alimuomba Mkuu wa mkoa huo kusaidia kutatua vikwazo vinavyowakabili hususani mifugo barabarani na suala la wakandarasi.
Alisema kipo kikwazo cha wakandarasi ambao kutokana na miradi kuongezeka mingine inatekelezwa kwa kusuasua.