********************
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mwanaidi Ali Khamisi amewataka wanawake nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki Sensa ya watu na Makazi ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango ya kimaendeleo.
Aidha amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake ya kuwaamini wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi huku akiwataka wanawake hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii kwa lengo la kumsaidia Rais ili aweze kutimia majukumu ya kulijenga Taifa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwanaidi alisema kimsingi Sensa ya watu na makazi inapaswa kuungwa mkono na wananchi wote kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
“Nawasihi wanawake wenzangu kuona umuhimu wa kushiriki katika sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu, kimsingi zoezi hili ni muhimu kutokana na faida zake hasa linapokuja suala la maendeleo ya nchi” alisema Mwanaidi
Aidha kuelekea katika kilele cha siku ya wanawake Duniani Machi 8 Mwaka huu, yenye kaulimbiu isemayo ‘ Kizazi chenye haki ya usawa kwa Maendeleo Endelevu, tujitokeze kwa wingi siku ya kuhesabiwa.
Naibu Waziri huyo alisema Tanzania inashuhudiwa ikiendelea kupiga hatua siku hadi siku chini ya Rais Samia.
Alisema chini ya uongozi wa Rais huyo, sekta mbalimbali zimeendelea kukua ikiwemo miradi ya kiuchumi ambayo kimsingi inazidi kuitangaza Tanzania kimataifa sambamba na kupunguza tatizo la umasikini.
“Tunapaswa kuendelea kumuunga mkono Rais wetu, amekuwa kiungo mzuri katika kuhakikisha Tanzania na watanzania wanasonga mbele, huyu ni mfano wa Mama bora ambaye anapambana kwa ajili ya familia yake” alisisitiza Mwanaidi
Pamoja na hayo alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akishiriki katika mikutano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa huku wakati wote akisimama na kuzungumzia vizuri Tanzania jambo linaloyavutia mataifa hayo ambayo baadhi yamevutiwa kuja kuwekeza nchini.