Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange akizindua jukwaa la Baraza la mazingira la Mkoa wa Manyara, Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Charles Makongoro Nyerere, kushoto ni Mratibu wa mtandao wa vikundi vya wakulima Manyara (MVIWAMA), Martin Pius na Ofisa kilimo wa sekretarieti ya Mkoa huo Samwel Dahaye.
…………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Manyara
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amezindua jukwaa la Baraza la wadau wa mazingira la Mkoa wa Manyara.
Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange akizindua jukwaa hilo kwa niaba ya Mkuu huyo wa Mkoa Makongoro amesema zaidi ya ekari 400,000 za misitu nchini huharibiwa kila mwaka, hali inayochangia uharibifu wa ardhi na vyanzo vya maji.
Twange akizindua jukwaa hilo lenye kauli mbiu ya kuimarisha ushirikiano katika hifadhi ya mazingira endelevu Manyara, amesema uharibifu huo wa misitu husababisha mabadiliko ya tabia nchi.
Ameliagiza jukwaa hilo kuweka mikakati yao wajikite kwenye kuwezesha upatikanaji wa teknolojia ya nishati mbadala na majiko banifu na kuelimisha jamii juu ya matumizi hayo.
“Wadau wa mazingira wahamasishe jamii kurejesha taka na kutambua fursa zilizopo ziwe na usimamizi endelevu wa taka, kuendesha kampeni za upandaji miti,” amesema Twange.
Amesema pia watunze vyanzo vya maji, kufanya kilimo endelevuq kinachozingatia utunzaji wa mazingira na kuhifadhi misitu ya asili ili kuzuia upotevu na uharibifu wa bioanuai.
Mratibu wa mtandao wa vikundi vya wakulima mkoa wa Manyara, (MVIWAMA) Martin Pius amesema Mkoa huo na maeneo mengine duniani, tayari umekumbwa na changamoto mbalimbali ya matokeo ya uharibifu wa mazingira.
Pius amesema hivi karibuni kulitokea ukame uliosababisha mifugo zaidi ya 65,000 kufa wilayani Simanjiro na Kiteto, kwa kukosa maji na malisho.
Amesema ni kwa sababu hiyo serikali imeona ni vyema kuita wadau wanaojishughulisha na kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira Manyara kuona namna ya kuunda jukwaa hilo.
“Tutaangalia namna ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na uharibifu wa mazingira, kujadili namna ya kushirikiana, kujenga uwezo na kubadilishana ujuzi na uzoefu,” amesema Pius.