Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu, leo Machi 4, 2022 wamefutiwa mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Mbowe na wenzake wameachiwa baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, DPP, kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo hatua ambayo imepelekea Mbowe na wenzake watatu kuachiliwa huru mara moja.
Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilikuwa imemshikilia Mbowe na wenzake watatu kwa kesi ya kujibu kuhusiana na tuhuma mbalimbali zikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi.
Taarifa ya kuondoa mashtaka iliwasilishwa na wakili wa serikali. “Mheshimiwa Jaji Taarifa Hii tunaiwasilisha kwa Njia ya Maandishi, Kwa Maombi hayo ya Kifungu cha 91(1) tunaomba Kuondoa Mashitaka Yote dhidi ya Washitakiwa Wote Sababu zote zipo katika Noel Prosecui ambayo tumeiwasilisha” alisema wakili wa serikali mbele ya jaji Joachim Tiganga ambaye amekua akisimamia kesi hiyo.