Naibu Katibu Mkuu ( Afya), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Grace Magembe ameagiza kupatiwa orodha ya majina ya Waganga Wakuu wa Halmashauri ambao wameshindwa kutoa mafunzo ya ukaguzi wa bidhaa za afya kwa timu ya uendeshaji ya Halmashauri zao ili hatua zichukuliwe.
Agizo hilo amelitoa leo Machi 4, Mwaka 2021 kwenye majumuisho ya ziara yake aliyoifanya katika Halmashauri za Gairo na Mvomero mkoani Morogoro iliyolenga kukagua ubora wa utoaji wa huduma ya Afya na ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma inayoendelea kujengwa.
Dkt.Magembe ametoa agizo hilo kwa Mkurugenzi wa huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii wa TAMISEMI kuwasilisha orodha hiyo ili wapangiwe kazi nyingine kwa kuwa wamekosa sifa ya kuwa Wakuu wa Idara.
“ Nilitoa maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Halmashauri kutoa mafunzo ya ukaguzi wa dawa, vitendanishi vya maabara na vifaa tiba kwa timu ya uendeshaji wa Halmashauri sasa wale ambao bado hawatoa hayo mafunzo Mkurugenzi wa huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii niwasilishie orodha ya wote ambao hawajatekeleza,” amesema.
Sambamba na hilo, Dkt. Magembe amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio kuwasilisha taarifa ya ukaguzi wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba katika Kituo cha Afya Sabasaba kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Hospitali ya Wilaya Mvomero ndani ya siku saba kuanzia leo.
“Sijaridhishwa na taarifa ya bidhaa za afya katika Kituo cha Afya Sabasaba na Hospitali ya Wilaya Mvomero, nikuagize Mganga Mkuu wa Mkoa ndani ya siku saba nahitaji ripoti ya ukaguzi,” amesema Dkt.Magembe
Amesema ukaguzi wa bidhaa za afya lazima ufanyike katika kila kituo cha kutolea huduma ya afya ili kudhibiti matumizi lakini pia kurahisisha ufatiliaji na usimamizi wa bidhaa hizo.