Mkuu wa wilaya ya Monduli ,Frank Mwaisumbe akizungumza katika wiki ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani itakayofanyika Machi 8,mwaka huu
Mkuu wa chuo cha maendeleo ya jamii Monduli, Elibariki Ulomi akizungumza katika wiki hiyo ya maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani itakayofanyika kitaifa Machi 8 .
…………………………………….
Happy Lazaro, Arusha
Mkuu wa wilaya ya Monduli ,Frank Mwaisumbe ameyataka madawati ya kijinsia nchini kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia kwa jamii za wafugaji ili zifahamu haki zao kwani zimekuwa zikikutana na changamoto nyingi kutokana na Mila na desturi zao.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza katika wiki ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani inayotarajiwa kufanyika Machi 8, sambamba na uzinduzi wa dawati la jinsia katika chuo cha maendeleo ya jamii Monduli .
Mwaisumbe amesema kuwa, kuna haja kubwa kwa madawati hayo kutumika ipasavyo katika kutoa elimu ya jamii hiyo kutokana na Mila potofu ambazo zimekuwa zikiwakandamiza wanawake wa jamii hiyo.
“naomba haya madawati yakawe chachu ya mabadiliko katika jamii zinazowazunguka kwa kutoa elimu ya kutosha juu ya kupinga ukatili ya kijinsia huku kila mmoja akizifahamu haki zake na kuweza kuondokana na ukatili huo.”amesema .
Mwaisumbe amesema kuwa, wilaya za kifugaji ni moja kati ya wilaya zilizoathirika na unyanyasaji wa kijinsia kutokana na mila na desturi zao ,hivyo kupitia madawati hayo wataweza kupata elimu na ufahamu wa kutosha sehemu ya kukimbilia pindi wanapokutana na changamoto Kama hizo na kuweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Aidha ameyataka madawati hayo kutobagua watu wa kuwapa haki bali watoe haki kwa makundi yote wakiwemo wanaume kwani wapo wanaofanyiwa ukatili kwa kiwango kikubwa ila hawana sehemu sahihi ya kusemea mambo yao.
Naye Mkuu wa chuo cha maendeleo ya jamii CDTI Monduli, Elibariki Ulomi amesema kuwa,chuo hicho kimeweza kuanzisha vikundi 10 vya wanajamii ambapo kila kikundi kina mradi wa kujiongezea kipato ,ambapo kupitia VICOBA wameweza kuhamasisha wanajamii kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba bora mbili.
Amesema kuwa, kuzinduliwa kwa dawati hilo ni chombo kitakachotumika kuibua na kuchochoea ari ya uelewa wa masuala ya kijinsia katika maeneo mbalimbali ya upatikanaji wa fursa na huduma pamoja na kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Taasisi na jamii inayotuzunguka.
Mratibu wa kitengo hicho cha dawati la jinsia CDTI Monduli, Beatrice Dominic amesema kuwa,dawati la jinsia ni kitengo kipya kilichoanzishwa chuoni kufuatia maelekezo ya serikali juu ya uanzishwaji wa madawati hayo katika vyuo vikuu na vya kati ambapo madawati hayo yanatoa fursa kwa Taasisi za mafunzo kuwa na uelewa mpana kuhusiana na masuala ya kijinsia .
Amesema kuwa, kupitia dawati hilo litakuwa likihudumia makundi yote ya jamii wakiwemo wanawake,wanaume na watu wenye mahitaji maalumu katika kuhakikisha wote wanakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mgawanyo wa majukumu ,fursa na upatikanaji wa huduma kulingana na makundi ya jamii,ambapo wamekuwa wakitoa elimu kwa wanawake hao na kuweza kuzifahamu haki zao huku wengi wao wakiweza kujitegemea kwa kufanya shughuli mbalimbali vya kujipatia kipato.
Mmoja wa wanawake hao,Noonguta Labahati amesema kuwa, kupitia chuo hicho wameweza kuondokana na mila potofu za kutegemea wanaume badala yake sasa hivi wanashiriki kikamilifu katika swala la maendeleo katika jamii zao,na hivyo kuweza kupunguza maswala ya unyanyasaji waliyokuwa wakifanyiwa na wanaume hapo awali ,kabla ya hawajazijua haki zao.