Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Paul Kimiti (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, upande wa kulia ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi hiyo Balozi Mstaafu Francis Mndolwa.Mjumbe waTaasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Bi. Ummy Wenceslaus akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
**********************
Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inatarajia kufanya makongamano ya kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kumbumkumbu ya miaka miamoja tangu Kuzaliwa kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Paul Kimiti, amesema kuwa ifikapo Aprili 13 Baba wa Taifa atakua anatimiza miaka100 tangu kuzaliwa, hivyo makongamano hayo yatafanyika kikanda yakienda sambamba na kufanya shughuli za kumuenzi baba wa Taifa pamoja na Upandaji wa miti.
Amesema kuwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi ya uhai wake alisimamia falsafa ya kulinda amani, kuondoa ubaguzi, na kuwafanya watanzania waweze kuishi kwa upendo na kujitegemea.
Amesema kuwa falsafa hizo zinapaswa kuenziwa kupitia Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu nyerere ili kuwafanya vijana na jamii kwa ujumla kuzifahamu.
Mwekiti Kimiti ameongeza kuwa wanapaswa kuendelea kuzijua kazi alizozifanya baba wa Taifa katika kulikomboa Taifa na kwamba kuenzi juhudi hizo kutalifanya Taifa kuendelea kulinda misingi ya amani, mshikamano na upendo na kuondoa ubaguzi miongoni mwa jamii ya kitanzania.
“Mwalimu Nyerere angekua hai April 13 anatimiza miaka mia moja tangu Kuzaliwa kwake, tumeamua kufanya kumbukumbu ya Kuzaliwa kwake kwa kufanya makongamano ambayo yatafanyika kikanda na tutafanya shughuli Mbalimbali za kumuenzi kikanda” amesema Kimiti.
Ameeleza kuwa watanzia kanda ya Ziwa pale Butiama alipozaliwa, kanda ya kati, kanda ya kaskazini, kanda ya kati Dodoma, Dar es salaam, Kanda ya kusini pamoja na kanda ya Magharibi.
Amefafanua kuwa kila kanda watafanyika shughuli za upandaji miti pamoja na makongamano yatakayozungumzia falsafa za mwalimu kulingana na historia ya mikoa iliyopo kwenye kanda hizi na jinsi ilivyohusika katika kuendeleza kudumisha amani, upendo na mshikamano.
Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo Simon Lubugu, amesema kuwa viongozi waliopo kwa sasa ni wale waliozaliwa miaka ya hivi karibuni, hivyo hawajui misingi ya baba wa Taifa ilivyokua.
Amesema kuwa kupitia Taasisi hiyo watapata fulsa ya kujua misingi ya Baba wa Taifa aliyowajengea watanzania email ya uhai wake.
“Viongozi wengi wa sasa wamezaliwa miaka ya themanini, hivyo wamekua sio wazalendo kwa Taifa kwa sababu hawajui misingi iliyoachwa na muasisi wa Taifa hili” amesema Bw. Lubugu.
Amesema kuwa kuanzishwa kwa Taasisi hii itasaidia sana vijana waliozaliwa kipindi hiki na kijacho kufahamu misingi hiyo iliyoachwa na Baba wa Taifa.
Mjumbe wa Taasisi hiyo Ummy Wenceslaus, amewataka vijana kuona umuhimu wa kujiunga na Taasisi kutokana na mchango wa baba wa Taifa hili na mataifa mengine hasa katika kujenga misingi ya amani, mshikamano na upendo miongoni mwa watanzania.
Amewataka wasanii kutumia sanaa zao kupaza sauti juu ya kumuaenzi baba wa Taifa katika jamii ili kuendeleza mazuri ambayo ameacha Kama alama ya upendo kwa Taifa, huku akiwaasa pia viongozi kuyaishi kwa vitendo yale yote aliyoanzisha baba wa Taifa.
“Ni vyema viongozi wa sasa waishi falsafa ya baba wa Taifa kwa vitendo kwani falsafa zake zimesaidia kuleta ukombozi kwa Taifa na mataifa mengine Barani Afrika” amesema
Hata hivyo wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Taasisi hiyo, Balozi Mstaafu Francis Mndolwa, pamoja na Mhamasishaji Mtiti Mbassa Jirabi ambao kwa nyakati tofauti wameelezea umuhimu wa kumuenzi baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere.