Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara (Mb.) Mhe. Dkt Ashatu Kijaji amesema Tanzania imepata mafanikio makubwa kwa kushiriki Maonesho ya Dubai Expo2020 ambapo ilitia saini Hati za Makubaliano 36 katika uwekezaji katika sekta zote za kiuchumi zenye thamani ya Trioni 17.35 na ajira zaidi ya 200,000 zinazotarajiwa.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo wakati akiongea katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Kituo cha Clouds Machi 2, 2022 kuhusu mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushiriki wa Tanzania katika maonyesho ya Expo 2020 dubai yaliyoanza Oktoba 1, 2021 hadi Machi 31, 2022.
Akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza fursa za uwekezaji Tanzania, Siku ya Tanzania na kuongea na Watanzania waishio nchini humo, Dkt Kijaji amesema wawekezaji hao kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kushirikiana na wawekezaji wa Tanzania wanatarajia kufika nchini wiki ya pili ya mwezi Machi 2022 ili waanze utekelezaji wa makubaliano hayo kwa kuanza kufuata sheria za uwekezaji zilizopo ikiwemo usajili wa makampuni hayo nchini.
Dkt. Kijaji pia ameeleza kuwa Hati hizo za Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na UAE, na Sekta binafsi ya Tanzania na UAE zimefanyiwa uchunguzi yakinifu na kupitiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuhakikisha hakuna wawekezaji wababaishaji na kuwa Sheria zote za uwekezaji hususani zinazowalinda wawekezaji wa ndani zimefuatwa kabla ya kutiwa saini.
Aidha, Dkt Kijaji amewahakikishia wawekezaji kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji Biashara ikiwemo upunguzaji wa tozo mbalimbali ili kuvutia na kuwawezesha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hivyo wasisite kutumia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini ili kufikia malengo ya taifa ya kuifanya Tanzania kuwa kitivo cha Uwekezaji.
Akielezea Utayari wa Tanzania (Tanzania is ready to Take off) kupokea uwekezaji huo, Dkt. Kijaji amewaasa watendaji katika ngazi zote watakaohusika na wawekezaji hao kufanya kazi kwa uadilifu, bidii, weledi na ubunifu ili kuwezesha uwekezaji huo kwa ufanisi na kupata matokeo chanya yaliyotarajiwa katika ukuaji wa uchumi.