Mkuu wa Shule ya Sekondari Kilimani, Gerana Majaliwa,akizungumza wakati wa kuhitimisha michuano ya Khamese Sports and Games Bonanza.
Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Sekondari Kilimani,Atanas Manyika akifafanua umuhimu wa bonanza la Khamese Sports and Games.
Mwanafunzi wa kidato cha kwanza Kilimani sekondari,Groly Joseph akionyesha kipaji cha kuimba,aliimba nyimbo mbili ukiwa ni utunzi wake mwenyewe.
Mgeni rasmi, Mary Shama,akimkabidhi zawadi ya beberu la mbuzi mwalimu Abdallah Mzomwe baada ya timu kushinda mabao 3-1 dhidi ya Issa Shabaan. Picha zote na Baltazar Mashaka
…………………………………………………………….
NA BALTAZAR MASHAKA,Ilemela
SHULE ya Sekondari Kilimani,imeanzisha michuano ya Khamese Sports and Games Bonanza ili kuibua vipaji,kujenga uwezo wa wanafunzi wa kitaaluma,kudhibiti utoro na kuimarisha uhusiano na walimu.
Mkuu wa Shule hiyo, Gerana Majaliwa,akizungumza jana wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi,alisema ili kutimiza malengo waliyojiwekea kitaaluma (kuinua ufaulu) na kimichezo, michuano hiyo itakuwa endelevu.
Alisema wameanza na michezo ya soka,pete, wavu,drafti,maonyesho ya kitaaluma na mavazi,kuimba,sarakasi,dansi na vichekesho ili kuwapa wanafunzi burudani badala ya taaluma pekee ili kuwajenga kisaikolojia,kiakili na kimwili.
“Bonanza la Khamese Sports and Games ni endelevu,limeanzishwa kuibua na kutambua vipaji vya watoto na kuviendeleza,kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujifunza,kudhibiti utoro na kuchochea watato kuipenda shule,kuimarisha uhusiano chanya kati ya walimu na wanafunzi,tunaamini ufaulu na taaluma itainuka zaidi,”alisema Majaliwa.
Pia bonanza hilo linalenga kutambua na kuenzi mchango wa Mwenyekiti wa Bodi ya shule kwa miaka 8,pia Diwani wa zamani wa Pasiansi (CCM) na Meya wa Jiji la Mwanza,Ramadhan Khamese,aliyejenga shule hiyo kabla ya kuikabidhi jiji.
Mgeni rasmi wa bonanza hilo,Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyasaka,Mary Shama,akikabidhi zawadi kwa washindi alisema likiendelezwa litaibua vipaji vingi na kuwataka wanafunzi kujikita kwenye taaluma,wazingatie nidhamu na utii kwa walimu ili kufaulu masomo.
“Kwa mwanafunzi elimu inakuwa haina mwisho unapoiendeleza shuleni si uwe mitaani halafu unaibuka baada ya miaka 20,mwenye nidhamu na utii anatafanikiwa kwenye masomo hivyo jiepusheni na uhusiano usiofaa,heshimianeni walimu na wanafunzi,”alisema.
Aidha timu ya soka ya mwalimu Abdallah Mzomwe,imetwaa ufalme wa mchezo huo kwa kuilaza Issa Shaaban mabao 3-1 na kuzawadiwa beberu la mbuzi.
Timu ya Maugo Malima ilitwaa umalkia wa mchezo wa mpira wa pete kwenye bonanza hilo kwa kuichakaza pete 6-2, timu ya mwalimu wa michezo,Mary Bwire na kujinyakulia mbuzi beberu.
Timu nyingine ni ya mpira wa wavu ya Issa Shaaban iliichapa Mugendi Mugwe kwa seti 3-0 na upande wa drafti timu ya Lazaro Anthony iliitambia Mzomwe na kutwaa zawadi ya kuku jogoo.
Upande wa usafi bweni la Brilliant likiongozwa na Liberata Kabage,liliibuka mshindi na kunyinyakulia zawadi ya jogoo la kuku likiyabwaga mabweni ya Sokoine,Precious na Winners.