…………………………………
Na John Walter-Babati
Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Manyara limepongezwa kwa kuwahudumia wananchi wa mkoa huo kwa kuwafuata katika maeneo yao, kuwasikiliza na kutatua changamoto zao.
Pongezi hizo zimetolewa na mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange wakati akipokea Msaada wa Vitanda ishirini vya wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Mutuka yaliyotolewa na Shirika lisilo la kiserikali la Maisha Capacity Development Opportunity (MCDO).
Twange amesema tangu meneja mpya wa Tanesco Mhandisi Fadhili aanze kazi katika mkoa wa Manyara mambo yamebadilika ikiwemo malalamiko ya wananchi kupungua kwa kuwa menja kila siku anawatembelea wananchi na kuzungumza nao huku akishirikiana vyema na viongozi mbalimbali ngazi ya mkoa,wilaya hadi vijiji.
Mbunge wa Jimbo la Babati mjini Paulina Gekul (Naibu waziri wa Utamaduni,sanaa na Michezo) amesema kwa kasi ya TANESCO kwa sasa wananchi wataacha kumsumbua kuhusu umeme kwani amekuwa akipata ushirikiano mzuri kutoka Viongozi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Babati Mjini Elizabeth Malley amesema Meneja huyo anahitaji pongezi kwa kuwa ni mchapakazi na kwamba chama hicho kinahitaji watu wa aina hiyo.
Nao baadhi ya wananchi wamesema Shirika hilo kwa sasa limebadilika tofauti na awali ambapo hapakuwa na mfumo wa utoaji taarifa kuhusu kukatika kwa umeme, ila kwa sasa hata kama kuna katizo la umeme wamekuwa wakipata taarifa mapema na wao kujipanga hivyo kuondoa usumbufu.
Meneja wa Shirika la Umeme (TANESCO katika mkoa wa Manyara ameendelea kutoa elimu kwa wananchi kwenye vijiji na mitaa juu ya gharama mpya za kuunganisha umeme maeneo ya mijini na vijijini ambapo wananchi wanapata nafasi ya kuuliza maswali na kupatiwa majibu.
Aidha amewataka wananchi wenye changamoto ya namba ya malipo (Contoll number) wawasiliane na viongozi wao wa mitaa na vijiji ili wapatiwe ufumbuzi wa tatizo hilo mapema.