**************************
Na. John Mapepele
Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Hassan Abbas amesema Tamasha kubwa la kihistoria la Muziki lijulikanalo kama Serengeti Music Festival la mwaka huu limeongeza siku ambapo sasa litafanyika kwa siku mbili badala ya moja kama ilivyopangwa awali kutokana na mahitaji makubwa ya tamasha hilo kwa wasanii na wananchi.
Akizungumza na Kamati ya Maandalizi yaTamasha hilo leo Machi 1, 2022 jijini Dar es Salaam amesema kuongezeka kwa siku hizo kunatokana na wasanii wengi kuomba kushiriki katika tamasha la mwaka huu ambalo litafanyika kuanzia Machi 12-13, 2022 jijini Dodoma.
“Mwitikio wa wasanii tulioupata katika msimu huu ni mkubwa sana ambapo hadi sasa wasanii wakongwe na chipukizi zaidi ya mia moja wameomba kushiriki tamasha hili kutokana na jinsi ambavyo limekuwa likiandaliwa vizuri na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali” . Amefafanua Dkt. Abbas
Aidha, Dkt. Abbasi amesema kuwa Tamasha hili ndiyo tamasha pekee kubwa linalowaleta pamoja wasanii mbalimbali, wachanga na wakongwe, pia bendi za muziki kujumuika pamoja bila kujali lebo zao.
Ameongeza kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha wasanii wanabadilishana uzoefu kwenye fani ya muziki ili kukuza vipaji vyao huku wakitumia tamasha hilo kutangaza utalii na vivutio mbalimbali vya Tanzania.
“Tamasha hili tumelipa jina la Serengeti kwa dhumuni la kuonyesha na kurithisha sanaa ya muziki kwa vizazi vya sasa na baadaye lakini pia kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya utalii kupitia Mbuga ya Serengeti .” Ameongeza Dk. Abbas
Pia amesema tofauti na matamasha mengine wasanii wote wanaoshiriki tamasha hili wanapata fursa ya kufundishwa na wataalam mambo mbalimbali kabla ya kufanya maonesho yao.