Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea Geofrey Mashafi kushoto akitoa taarifa kwa Jaji Mkuu Professa Ibrahim Juma kulia,kukosekana kwa Jengo la Mahakama ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma ambapo kwa sasa wanalazimika kutumia jengo la kukodi ambalo halina sifa ya kutumika kama kwa shughuli za Kimahakama,katikati Mkuu wa wilaya ya Nyasa Kanali Raban Thomas.
Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma kushoto akimpa zawadi ya Kalenda ya Mwaka 2022 Mkuu wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Kanali Raban Thomas mara baada ya Jaji Mkuu kuwasili wilayani Nyasa kwa ziara ya kikazi ya siku moja . Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma kushoto,akimsikiliza jana Mkuu wa wilaya ya Nyasa na Mwenyekiti wa kamati ya maadili ya Mahakama katika wilaya hiyo Kanali Raban Thomas kuhusu ukosefu wa Jengo la Mahakama ya wilaya ambapo kwa sasa watumishi wanatumia jengo la kukodi kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali za Mahakama.
****************
Na Muhidin Amri,
Nyasa
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,imesaini makubaliano na Benki ya Dunia kuendelea kuifadhili Mahakama ya Tanzania katika kuboresha miundombinu ya majengo katika awamu ya pili.
Katika makubaliano hayo, Mahakama inatarajia kujenga vituo jumuishi vingine vya Utoaji haki tisa katika mikoa isiyo na majengo ya Mahakama Kuu pamoja na Mahakama za Mwanzo 60 hapa nchini.
Hayo yamesemwa jana na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, wakati akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Nyasa akiwa katika ziara yake mkoani Ruvuma kuongea na watumishi na kuangalia maboresho ya miundombinu ya Mahakama iliyofanyika katika kipindi cha miaka mitano.
Alisema,hivi sasa ya Serikali na Benki ya Dunia zipo katika awamu ya mwisho ya makubaliano, ambapo maboresho hayo yatasaidia sana kumaliza baadhi changamoto ikiwamo majengo na miundombinu mbalimbali katika kipindi cha miaka minne ijayo.
Jaji Mkuu,ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha ambazo zimewezesha kufanya maboresho na mabadiliko makubwa ya Mahakama nchini katika muda wa miaka mitano iliyopita.
Amewataka watumishi wa Mahakama wilayani humo,kuendelea kuchapa kazi kuzingatia maadili na weledi mkubwa wakati wa kusikiliza mashauri na kutoa hukumu mbalimbali ili kuepuka malalamiko yasio ya lazima kutoka kwa jamii.
Aidha,ameipongeza Mahakama ya wilaya ya Nyasa kwa kufanikiwa kuondosha(kusikiliza)mashauri kwa asilimia 88 kuanzia Mwezi Januari hadi Disemba 2021 licha ya wilaya hiyo kuwa na Hakimu mmoja,huku Mahakama ya za Mwanzo zikifanikiwa kumaliza mashauri yaliyofikishwa kwa asilimia 97.
Amewapongeza watumishi wa Mahakama katika wilaya ya Nyasa kwa kazi nzuri wanayofanya,lakini amewataka kujiandaa na mabadiliko na matumizi ya Tehama katika utendaji wa kazi za kila siku badala ya utaratibu wa zamani wa kutumia karatasi.
Alisema,kwa sasa Mahakama hapa nchini ina upungufu wa watumishi takribani laki sita,lakini kwa kutumia mfumo waTehama utasaidia kupunguza pengo hilo na kuwataka kujiendeleza kielimu ili kwenda sambamba na mabadiliko makubwa yanayofanywa na Mahakama.
Katika hatua nyingine Jaji Mkuu alisema,kuanzia mwezi Juni mwaka huu Serikali inatarajia kujenga majengo ya Mahakama katika wilaya mbalimbali hapa nchini ikiwamo wilaya Nyasa kwa ajili ya kutoa huduma za Kimahakama kwa watumishi na wananchi.
Kwa upande wake Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea Geofrey Mashafi alisema,Halmashauri ya wilaya ya Nyasa imeshatoa kiwanja chenye ukubwa wa mita za mraba 16,920 tangu mwaka 2017 ambacho kinafaa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya wilaya.
Kwa mujibu wa Mashafi, kwa sasa jengo linalotumika kama Mahakama ya wilaya ya Nyasa ni la kukodi la halipo katika hali nzuri,hivyo amemuomba Jaji Mkuu kutoa kipaumbele suala la ujenzi wa Mahakama katika wilaya hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Nyasa Kanal Raban Thomas alisema,kama Serikali itajenga jengo la kisasa la Mahakama katika wilaya hiyo itasaidia kuwapunguza wananchi usumbufu wa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta haki.
Kanali Thomas alisema, kama Serikali wanatakiwa kutenda haki na watahakikisha haki inapatikana kutoka kwenye vyombo na watumishi waliopewa dhamana na wajibu wa kutenda na kutoka haki.
MWISHO