Na John Walter-Babati
Wakazi wa kata ya Mwada wilaya ya Babati mkoani Manyara, sasa wataondokana na changamoto ya kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za afya na kupunguza gharama za usafiri baada ya Hospitali ya wilaya iliyopo katika kata hiyo kuanza kufanya kazi.
Hospitali hiyo ya Halmashauri ya wilaya ya Babati ilisubiriwa kwa hamu na wananchi haswa wale wa ukanda wa tarafa ya Mbugwe kwani walikuwa wakilazimika kwenda kupata huduma za matibabu katika mji wa Babati,Dareda na maeneo mengine ambapo ni mwendo mrefu.
Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka 2012 Halmashauri ya wilaya ya Babati ilikuwa na wakazi wapatao 312,392 ambapo kwa sensa inayotarajiwa kufanyika mwaka huu idadi hiyo ya watu inatazamiwa kuongezeka maradufu.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa katika ziara yake wilaya ya Babati Januari mwaka huu aliagiza ifikapo Machi 1,2022 hospitali hiyo iwe imeanza kufanya kazi, agizo ambalo limetekelezwa kwa wakati.
Akizungumza Jumanne Machi 1, 2022 mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amewatangazia wananchi wa wilaya ya Babati kuwa sasa huduma zimeanza kutolewa katika hospitali hiyo huku akiongeza kuwa vifaa na wataalamu wapo, hivyo hakuna haja ya kwenda mbali tena kufuata huduma.
Amesema mpango wa serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa karibu na kuwaondolea usumbufu wa kwenda umbali mrefu hali inayowarudisha nyuma kimaendeleo.
Wakazi wa kijiji cha Mwada Lusiana Paskali na Pauli Michael wameishukuru serikali kwa kupeleka mradi wa hospitali katika kata hiyo.
“Kwa kweli tunaishukuru sana serikali kwa sababu zamani tulikuwa hatuna huduma hasa kwa mama anapotaka kujifungua, ilikuwa lazima kwenda mjini Babati (Mrara) ambapo gharama za usafiri zilikuwa kubwa wakati wa kokodi usafiri hasa ikiwa usiku, wakati mwingine mama aliweza kujifungulia njiani,”
Mganga mkuu wa wilaya ya Babati Hosea Madama amesema Hospitali imeanza kutoa huduma za wagonjwa wa nje na huduma ya Maabara ambapo wameanza na wateja zaidi ya 14.
Hata hivyo Dr.Madama amesema wanategemea kuanza kutoa huduma zingine zikiwemo za Mionzi,Kulaza wagonjwa, Huduma za mama kujifungua na kadhalika.