Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imejipambanua kuwa imedhamiria kuboresha mazingira ili kutoa fursa kwa wadau kushiriki katika sekta mbalimbali, iwe siasa, biashara, uwekezaji au masuala ya usawa wa kijinsia.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Denmark anayehusika na Masuala ya Sera na Maendeleo, Bi. Lotte Machon jijini Dar Es Salaam tarehe 28 Februari 2022.
Balozi Mulamula alieleza kuwa tokea Rais Samia aingie madarakani Serikali yake imechukua hatua mbalimbali za kuboreha mazingira ya biashara na uwekezaji, kutoa uhuru zaidi wa kisiasa, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha ushirikiano na nchi za nje na mashirika ya kimataifa, kuboresha miundombinu na kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19.
Balozi Mulamula alieleza kuwa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Denmark umetimiza miaka 60 sasa, na katika kipindi hicho, nchi hizo mbili zimeshirikiana katika maeneo mengi ikiwemo Tanzania kufaidika na misaada ya Denmark katika sekta tofauti kama vile; huduma za afya, elimu, mabadiliko ya mifumo ya kodi, nishati, kilimo, athari za mabadiliko ya tabianchi, biashara na uwekezaji.
Mhe. Waziri alimuhakikishia Bi. Machon kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Denmark na kusisitiza umuhimu wa nchi hiyo kuendelea kuisaidia Tanzania hususan, kwa kuunga mkono jitihada za kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi wa Denmark kuja kuwekeza nchini ili pamoja na mambo mengine uwekezaji huo uweze kutoa ajira kwa vijana ambao idadi yao kwa nchi za Afrika ni kubwa.
Kwa upande wake, Bi. Machon alielezea utayari wa Denmark kuendelea kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo tofauti yakiwemo ya demokrasia, nishati na mabadiliko ya tabianchi. Alisema nchi hiyo kila mwaka inatenga asilimia 1 ya pato lake kwa ajili ya misaada ya maendeleo kwa nchi marafiki ikiwemo Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Denmark anayehusika na Sera na Maendeleo, Bi. Lotte Machon jijini Dar Es Salaam.
Ujumbe aliongozana nao Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Denmark anayehusika na Sera na Maendeleo, Bi. Lotte Machon ukinukuu dondoo muhimu za mazungumzo.
Ujumbe wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ambao kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Ulaya na Amerika Balozi Swahiba Mndeme,, Afisa Dawati, Bi. Kisa Mwaseba na Katibu wa Waziri, Bw. Seif Kamtinda.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akitoa maelezo ya zawadi aliyomkabidhi Katibu Mkuu wa Denmark.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberat Mulamula (Mb) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Denmark anayehusika na Sera na Maendeleo, Bi. Lotte Machon wakiwa katika picha ya pmoj na ujumbe wao.