******************
Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amewapongeza watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mbio za Kilimanjaro Marathon na kuongoza katika mbio hizo tofauti na miaka ya nyuma ambapo mataifa mengine yamekuwa yakiongoza.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo, Februari 28, 2022 na kufafanua kuwa mwitikio huo mkubwa umetokana na kazi nzuri ambayo iliyofanywa na Rais wa Samia Suluhu Hassan toka akiwa Makamu wa Rais ambapo aliongoza kuhamasisha riadha na kuanzishwa kwa klabu za mazoezi (jogging clubs) kwenye kila mkoa hapa nchini.
Aidha amesema mikakati kabambe iliyowekwa na Serikali ya sasa kwenye Sekta ya michezo inakwenda kuleta mapinduzi makubwa ikiwa ni pamoja na kutoa ajira nyingi kwa wananchi.
Katika mashindano hayo mtanzania Alyce Simbu aliongoza kilomita 42 aliyetumia muda wa 02:16:30 wakati kwenye kilomita 21 nafasi ya kwanza hadi ya tatu zilichukuliwa na watanzania zikiongozwa na Emmanuel Ginniki (01:00:34), akifuatiwa na Gabriel Geay (01:02:04) na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Inyasi Sulley(01:04:10).
Akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya Kili Marathon jana Februari 27, 2022 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha sekta ya michezo nchini inapiga hatua kwenda mbele kwani michezo ni zaidi ya burudani.
Ameshauri mbio hizo ziitwe Kilimanjaro International Marathon kwa kuwa zinashirikisha mataifa mengi duniani.
Pia aliziagiza Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii zishirikiane na waandaaji ( Executive Solution) wa Kilimanjaro Marathon kuona jinsi ya kutumia tamasha hili kutangaza zaidi fursa za utalii na vivutio mbalimbali kimataifa.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Riadha nchini Silas Lukas ameishukuru Serikali kwa kuweka kipaumbele kwenye riadha na kusema Shirikisho litahakikisha mchezo wa riadha unazinazidi kukua na kuchangia kwenye uchumi wa nchi yetu.