Na Lucas Raphael Igunga
Kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika kijiji cha Mwalala kata ya Nguvumoja wilayani Igunga mkoani Tabora imeharibu miundombinu ya barabara vibaya kutoka kijiji cha Mwanzugi kwenda kijiji cha Mwalala na kusababisha wananchi wa kijiji cha Mwalala kukosa mawasiliano kutokana na barabara hiyo kusombwa na maji baadhi ya maeneo.
Diwani wa kata ya Nguvumoja Gedi Nkuba CCM alisema barabara hiyo ilisombwa na maji kutokana na madaraja yaliyojengwa katika barabara hiyo kuzibwa na uchafu unaosababishwa na baadhi ya wakulima wanaolima kwenye hifadhi ya barabara pasipo kuchoma moto uchafu wanaosafisha kwenye mashamba yao.
Alisema hivi sasa wananchi wa kijiji cha Mwalala wanashindwa kufika mjini Igunga kupata huduma za kijamii kufuatia barabara hiyo kutopitika kabisa huku baadhi ya wagonjwa wanaotakiwa kwenda kupatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Igunga wakishindwa kufika.
Aidha Diwani huyo alibainisha kuwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kukarabati maeneo yaliyosombwa na maji wananchi wa kijiji cha Mwalala wataendelea kuteseka ikiwa pamoja na kukosa huduma za matibabu kutokana na zahanati ya kijiji hicho kukosa dawa kwa kuwa hakuna uwezekano wa gari la kubeba dawa kupita eneo hilo.
Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mwalala Kasule Kasandiko, Milembe Jihambo, Ashura Njile na Masunga Nindwa wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema kutokana na barabara hiyo kusombwa na maji wamekuwa wakipata adha ya kutafuata huduma za kijamii katika kijiji cha Mwanzugi huku wakibainisha changamoto kubwa imekuwa ikitokea nyakati za masika kwani baadhi ya wakulima wamekuwa na tabia ya kulima kwenye hifadhi ya barabara huku wakisafisha mashamba yao pasipo kuchoma uchafu wa miti.
Hata hivyo wananchi hao waliiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria wakulima ambao wameendelea kulima kwenye hifadhi ya barabara wakati walishapewa elimu na viongozi wa TARURA wilaya ya Igunga kuacha tabia ya kulima kwenye hifadhi ya barabara na kuongeza kuwa bila kuchukua hatua madaraja yanayojengwa yataendelea kuziba na uchafu.
Nae mbunge wa jimbo la Igunga Nicholaus Ngassa aliyefika katika eneo hilo la kijiji cha Mwalala ambako barabara imesombwa na maji alisema changamoto aliyoikuta hapo ya kusombwa barabara na maji ni kwa sababu midomo ya madaraja imeziba kutokana na uchafu jambo ambalo ililazimika baada ya mvua kunyesha maji yatafute sehemu nyingine ya kupita.
Mbunge Ngassa alisema tayari ameuagiza uongozi wa TARURA wilaya ya Igunga kuchukua hatua za haraka kumwaga mawe maeneo yote barabara iliyosombwa na maji ili wananchi waweze kupita huku akiwataka pia viongozi wa TARURA kuziondoa taka zote zilizopo kwenye midomo ya madaraja na kuzichoma moto.
Hata hivyo amewataka wananchi wa jimbo la Igunga kuacha tabia ya kulima mazao kwenye hifadhi za barabara kwani serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kujenga miundombinu ya barabara hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuzitunza barabara hizo.
Sambamba na hayo Mbunge Ngassa amewaagiza wenyeviti wa vitongoji, watendaji wa vijiji, kata na madiwani wote wa jimbo la Igunga kuendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yao juu ya kutofanya uharibifu katika hifadhi za barabara.
Kwa upande wake kaimu mhandisi wa TARURA wilaya ya Igunga Eng. Costantine Ibengwe alithibitisha barabara ya kijiji cha Mwalala baadhi ya maeneo kusombwa na maji ambapo alibainisha kuwa chanzo cha maji kushindwa kupita kwenye midomo ya madaraja ni uchafu unaotokana na wananchi wanaposafisha mashamba yao ya kulima hawachomi taka hizo.
Mhandisi Ibengwe alisema tayari wameanza kuchukua hatua za dharura kwa kuweka mawe na kutoa taka kwenye madaraja hayo, aidha mhandisi huyo alibainisha kuwa hadi sasa zinahitajika zaidi ya Mil. 200 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo, huku akitoa wito kwa wananchi kuacha mita 12 kutoka kwenye hifadhi ya barabara kufanya shughuli za kilimo.