*******************
Naibu Waziri wa Kilimo Mh Anthony Mavunde jana ametembelea ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na kukagua ujenzi wa jengo la maabara mpya ya kisasa inayojengwa na Serikali kwa gharama ya Shilingi Bilioni moja katika eneo la Kilimo 3,Chang’ombe Wilayani Temeke.
Maabara hii yenye hadhi ya kimataifa itakuwa ni moja kati ya maabara kubwa na bora katika ukanda wa Afrika Mashariki katika upimaji wa ubora wa mbolea.
“Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha tunakuza sekta ya kilimo na hasa katika kuwekeza kwa ukubwa kwenye eneo la pembejeo kuanzia upatikanaji wake mpaka ubora wake.
Maabara hii ikikamilika itasaidia sana kupunguza muda wa kusubiri majibu ya upimaji wa sampuli za mbolea tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo muda unaotumika kusubiri majibu ni mpaka miezi miwili kutokana na kwamba Mamlaka inategemea huduma ya Taasisi zingine za udhibiti ubora kwa upimaji wa ubora wa mbolea kabla majibu hayajamfikia mhusika.
Jengo linalojengwa liwe ni kitovu cha taarifa, huduma na habari zote (fertilizer one stop centre) zinazohusiana na mbolea nchini; maabara iwe ni ya kisasa na ya kuvutia na kituo cha ubora kuhusu masuala yote yanayohusu mbolea (fertilizer centre of excellence); na jengo liwe na nafasi kwa ajili ya wataalamu kutoka katika taasisi zingine zinazohusika na masuala ya pembejeo” Alisema Mavunde
Akitoa maelezo ya awali,Mkurugenzi Mkuu wa TFRA **Dr Stephan Ngailo **amesema jengo hilo la maabara linatarajiwa kukamilika mapema mwezi Mei,2022 na kukamilika kwake kutasaidia kuongeza ufanisi katika udhibiti wa ubora wa mbolea hapa nchini na pia maabara hiyo itakuwa chanzo cha mapato ya Serikali kwa kuwa wanategemea kuhudumia zaidi ya nchi tatu zinazoizunguka nchi ya Tanzania.