Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk.Gladness Temu akiwasilisha mada Jana kuhusu bioteknolojia kwa waandishi wa habari pichani hawapo.
Ofisa kutoka ofisi ya Makamu wa Rais, Thomas Chali akielezea kwa waandishi wa habari kuhusu Sera mpya ya Mazingira ya mwaka 2021.
Wadau na waandishi wa habari wakifuatilia kwa makini mafunzo
**********************
Na Mwandishi Wetu
WAANDISHI wa Habari nchi wameshauriwa kusoma na kuilewa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021, ili waweze kuainisha fursa zilizopo ndani yake.
Aidha waandishi wametakiwa kushiriki kwenye mashindano ya habari za kilimo sayansi hasa katika eneo la bioteknolojia.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uratibu na Usimamizi Uendelezaji wa Utafiti, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Bugwesa Katale mwishoni mwa wiki mkoani Dar es Salaam kwenye mafunzo kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu sera mpya ya mazingira na fursa na changamoto za bioteknolojia.
Katale alisema sera mpya ya mazingira imeainisha mambo mengi mazuri, ila ufanisi wake utaonekana iwapo waandishi wa habari na wadau wengine watachukua jukumu la kutoa elimu.
“Februari, mwaka huu Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, ambayo inalenga kuondoa mapungufu, vikwazo na changamoto zilizokuwamo kwenye Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997 ambayo ilikuwa na changamoto ya kukosekana kwa baadhi ya masuala muhimu Kwa maendeleo ya taifa,” alisema.
Alisema Sera mpya mpya imeboresha maeneo kadhaa na kuongeza fursa na kuruhusu matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni (Bioteknolojia) katika kilimo, afya na viwandani.
Akiwasilisha mada kuhusu ubunifu katika teknolojia ya uhandisi Jeni, Thomas Chali, kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, alisema baada ya sera kuzindiliwa Februari, mwaka huu, mwongozo umetolewa kuhusu teknolojia hiyo ikiwamo ulinzi wa mazingira hivyo kuwakaribisha watafiti kutumia fursa hiyo kutafiti.
Chali alisema changamoto zilizokuwamo kwenye Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997, ni pamoja na kukosekana mwongozo wa mabadiliko ya tabianchi, udhibiti wa taka ngumu, wadudu vamizi na matumizi ya uhandisi jeni ili kutengeneza dawa.
“Ongezeko la maisha ya kisasa, mwingiliano wa watu eneo moja hadi lingine inasababisha uharibifu wa mazingira,”alisema
Ofisa huyo alisema pia sera ya zamani ilikuwa hainishi matumizi mapya ya mbegu, bidhaa za kiteknolojia kuongezeka ikiwamo simu, televisheni kumeongeza uchaguzi na tatizo la kudhibiti taka zake,.
Alisema sera mpya imeibua fursa mbalimbali ikiwamo taka kubadilishwa kuwa biashara akitolea mfano bidhaa plastiki na chuma, zimeibua soko la chuma chakavu na urejelezwaji wa taka za plastiki viwandani.
“Awali sera haikuzingatia fursa katika mazingira. Sasa taka zilizoonekana kama tatizo ni fursa kibiashara, watu hivi sasa wanaokota makopo, chupa na kuuza, zamani watu hawa jamii iliwatafsiri kama vichaa, wendawazimu. Mtazamo kijamii umebadilika inaonekana shughuli hiyo ni ajira,” aliongeza Chali
Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaams (UDSM), Dk. Gladness Temu alisema teknolojia ya bioteknolojia inatumika katika maeneo mbalimbali duniani, hivyo Tanzania haiwezi kujitenga.
Temu alisema kinachohitajika ni kuwekeza kwenye elimu na utafiti ili kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa wa tenkonolojia hiyo.
“Bioteknolojia inatumika kwenye viwanda, afya na kwingineko. Ina changamoto zake lakini faida pia zipo, ili kuendana na dunia tunapaswa kuongeza nguvu kwenye utafiti,” alisema.
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Dk. Philbert Nyindodi ametoa rai kwa waandishi wa habari kote nchini kuandika habari za kilimo sayansi na kushiriki shindano ambalo linaratibiwa na COSTECH na OFAB.
“Changamoto za Uviko-19 na nyingine zilisababisha mwaka 2020 na 2021 tusishiriki shindano la habari za kilimo sayansi nawaomba kuanzia sasa muandike habari hizo na mwezi wa saba na nane tutakuwa tunatafuta mshindi,”alisema.