Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, akizungumza na wakazi wa Kisiwa Kome wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi akikagua kivuko cha MV Kome II kinachotoa huduma kati ya Nyakaliro na Kome katika Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya (aliyevaa kofia nyeupe), akijadiliana jambo na nahodha wa Kivuko cha MV Kome II mara baada ya kukagua kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Nyakaliro na Kome katika Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza. Kivuko cha MV Kome II kina uwezo wa kubeba tani 50.
Wakazi wa kisiwa cha Kome wakishuka katika kivuko cha MV Kome II ambacho kinatoa huduma kati ya Nyakaliro na Kome katika Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.
PICHA NA WUU
………………………………………………………
Wakazi wa Kisiwa cha Kome wilayani Sengerema wameiomba Serikali kuleta kivuko kingine kikubwa katika ukanda huo kwa kuwa kivuko kilichopo sasa cha MV Kome II hakikidhi mahitaji ya wakazi waliopo katika kisiwa hicho.
Wakazo hao wameeleza kuwa ongezeko la watu na shughuli za biashara ya samaki na dagaa zimechochea kuwa na mahitaji makubwa ya kivuko zaidi ya kimoja ili kusaidia kurahisisha utoaji huduma wa haraka.
Kivuko cha MV Kome II kinachotoa huduma ya usafirishaji mizigo na abiria katika Ziwa Victoria kati ya Nyakaliro na Kome katika Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kina uwezo wa kubeba tani 50 tu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, aliyefika katika kivuko hicho na kukagua shughuli zinazoendelea mahali hapo pamoja na kusikiliza changamoto za wakazi wa maeneo hayo.
“Kisiwa cha Kome kimeshakuwa kikubwa kwani kina wakazi takribani elf 20, hivyo tunaomba Serikali itusaidie kupata miundombinu wezeshi hususani kivuko kikubwa ili kuweza kukidhi mahitaji ya wananchi wa huku”, amesema Bw. Gidebanus Mutalemwa mkazi wa Kome.
Baada ya kusikia ombi hilo kwa wakazi hao, Kauli ya Serikali kutoka kwa Naibu Waziri huyo amewaahidi kulishughulikia suala hilo na kuagiza kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kuanza kufanya tathimini ya uwezo wa kivuko kitakachoweza kukidhi mahitaji ya wakazi wa hapo ili kuendana na hali halisi.
Vilevile amewataka TEMESA kuanza maboresho ya jengo la kusubiria abiria na majengo mengine mahali hapo ili wananchi wakae maeneo salama na yenye huduma zote wakati wanasubiria kuvuka.
“Wananchi niwatoe wasiwasi ombi lenu limefika na ndo maana nimefika hapa kujionea mahitaji ya wakazi wa eneo hili”, amesisitiza Eng. Kasekenya.
Naye, Kaimu Meneja wa TEMESA mkoa wa Mwanza, Eng. Atiki Abdallah, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa ongezeko la wakazi limefanya kivuko kilichopo kuzidiwa hivyo kuna umuhimu wa kupata kivuko kingine kikubwa ili kuboresha usafiri na usafirishaji kati ya haya maeneo kwa maana ya kuunganisha kisiwa cha Kome na ukanda wote wa Sengerema na Mwanza.
Ameongeza kuwa kivuko hicho kilichopo kimeongeza safari na muda wa utoaji huduma ambapo kwa sasa kwa siku kinavusha mara tano na ni kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 1 usiku tofauti na hapo awali.