********************
Na John Walter-Babati
Sheikh wa wa mkoa wa Manyara Mohammed Kadidi amesema kauli mbiu ya BAKWATA Taifa ,Jitambue, Badilika, Acha Mazoea imebadilisha mambo mengi ikiwemo viongozi ambao walikuwa wanaongoza waumini kwa mazoea.
Amesema hatarajii katika mkoa wa Manyara kumuona Sheikh wa kata au wilaya analalamikiwa badala yake anataka kuona wakiwa Chachu ya mabadiliko katika jamii wakishirikiana bila kubaguana.
Sheikh Kadidi ametoa wito huo leo Februari 26,2022 akizungumza na Masheikh wa kata mbalimbali za wilaya ya Babati na waumini wa dini ya kiislamu kwenye mashindano ya kuhifadhi Quran tukufu wilayani Babati yaliyofanyika katika msikiti wa BAKWATA mjini hapa.
Amemshukuru mkuu wa wilaya ya Babati kwa kushirikiana na BAKWATA katika shughuli zao mbalimbali wanazozifanya.
Amesema mashindano hayo ya kuhifadhi Quran tukufu ni agizo la Mufti na Sheikh mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Bin Zuberi Ali yanayosimamiwa na Baraza kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ambapo yanaanzia ngazi ya kata,wilaya,mkoa,kanda na Taifa.
Hata hivyo Sheikh wa mkoa wa Manyara Mohammed Kadidi ametoa wito kwa Waislamu wote na walimu wote wa Madrasa wajitahidi na kujipanga kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi kwa sababu mashindano hayo yatakuwa ni endelevu.
Kaimu Sheikh wa wilaya ya Babati Suleimani Idd Mussa amesema zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba kwa sasa wanajiandaa katika ngazi zinazofuata.
Washiriki kumi waliingia kwenye kinyang’anyiro ambapo kila mshiriki alipatiwa zawadi ya Juzuu huku mshindi wa kwanza hadi wa tatu akizawadiwa fedha taslimu na Juzuu.
Walioshinda kwa upande wa Kuhifadhi Juzuu tatu, wa kwanza ni Aziza Hassan, wa pili Ummliheri na wa tatu ni Alfadhili Idd.
Washindi katika Juzuu tano, wa Kwanza ni Mariam Lema, wa pili ni Omari Said na wa tatu ni Hamis Zuberi.