……………………………………..
Adeladius Makwega-DODOMA
Kwa hakika msomaji wa matini zangu kumbuka katika matini iliyotangulia niliyoipachika kichwa cha “Nyama hauli hata kama kisu unacho” nilizitazama aina tatu kati ya nne ya utani mgudini (Utani kazini).
Kwa leo mwanakwetu namalizia aina ya nne na ya mwisho.
Popote ulipo mwanakwetu, wewe jaribu kuitazama sehemu yako ya kazi, kwa hakika hata kama wewe si mpenzi wa mpira ni jambo la kawaida kuwatambua wafanyakazi /wafanyabiashara wenzako ambao ni wapenzi wa mpira. Utatambua tu fulani ni Simba na fulani ni Yanga.
Hali hii imekwenda mbali zaidi, kwa sasa hadi kumekuwa na mashabiki ya mipira wa timu za nje hasahasa timu za Uingereza kama vile Manchester United na Arsenall.
Kwa bahati mbaya mie mwanakwetu, kwa timu hizo za Uingereza sishabikii hata timu moja kati ya hizo mbili.
Mie timu yangu ni Newcastle united na jezi zake za zamani zilizokuwa zikifanana na kama punda milia enzi hizo za wachezaji kama mshambuliaji Joseph Kevin Keegan.
Ngoja niweke kando hizi habrai za soka la Ulaya.
Nakumbuka juma lililopita nilikuwa nazungumza ndugu yangu mmoja ambaye ni mzaliwa wa Kariakoo-Dar es Salaam ndugu huyu aliniambia kuwa Timu ya Yanga, mwanzoni makao yake makuu yalikuwa Mtaa wa Mafia. Kwa walio wengi wanatambua kuwa Yanga makao yake makuu ni mtaa wa Twiga kule Jangwani.
Shabiki huyu wa Yanga alisema kuwa hata kama Simba wana ofisi katikati ya Jiji hilo nao Yanga walikuwa na ofisini mjini.
Swali ambalo nilijiuliza je hiyo ofisi ya Yanga ya Mtaa Mafia kiwanja walipeleka wapi? Hilo mie halinihusu hayo ni mambo ya Yanga. Kama Yanga wanao jengo mtaa wa Mafia basi waamie hapo kama wanaweza.Maana Yanga wanataka kushindana na Simba kwa kila jambo.
Mwanakwetu huu ushindani wa michezo ndiyo aina ya nne ya utani kazini.
Mtafiti M Muya anasema kuwa timu za Mpira za Simba , Yanga na Cosmopolitani ni timu zilizokuwa na nguvu mno na utania mkubwa miaka ya 1970. Utani huo ulikuwa maradufu baina ya Simba na Yanga ambapo baadaye ikaundwa timu ya Nyota Nyekundu (Red Stars). Mtafiti M Muya katika utafiti wake wa utani wa mpira sehemu za kazini anasema kuwa maeneo mengi ya kazi huu utani unafanyika hasa hasa wakati wa mapumziko ya chai na chakula cha mchana, kwani kama mtu akifanya utani huo wakati wa kazi hilo halikubaliki.
“Wacha utani tufanye kazi bwana, kila saa mpira tu.”
Lakini wakiwa katika chai au chakula cha mchana katika mikahawa na magengeni hapo utasikia
“Ehh nani kafungwa jana”
Inawezekana kuwa jana hiyo, ilikuwa mechi baina ya Yanga na timu nyengine na muuliza swali pengine anayatambua matokeo hayo na labda Yanga imefungwa goli tatu mtungi
Shabiki huyo wa Yanga aliyeulizwa swali hilo anaweza kujibu, kwani wewe haukusoma katika gazeti? Nenda kasome Kisomo cha Watu Wazima. Anaweza kumalizia na kabila la mtu huyu, mathalani nyinyi Wakwere hamna akili kabisa.
“KIla mara serikali inasema nendeni mkasome nyie hamtaki, mnataka serikali iwafanyie nini?:”
Ukiyatazama majibu ya shabiki huyu wa Yanga kwanza kabisa ni kuyafupisha mazungumzo hayo, pengine kutokana na timu yake kufungwa goli tatu bila. Lakini shabiki mpinzani yeye anayaendeleza kwa utani huo.
Pia katika utani huo unamsikia shabiki wa Yanga anasema kuwa serikali inatoa elimu ya Watu Wazima nyie hamtaki kusoma.
Ndiyo kusema hata shughuli za maendeleo za taifa zinaweza kuelezwa vizuri kwa utani huo wa mpira.
Hata yule anayetaniwa kwa kuwa ameambiwa na shabiki pinzani anaweza kujirekebisha na akashiriki Kisomo cha Watu Wazima na kufuta ujinga. Hapa hata kama shabki wa Simba akawatania namna wachezaji wa Yanga wanavyoangukla mchezoni kama wana Kashakoo, hii itasaidia mashabiki hao kuona umuhimu wa lishe bora kwa jamii na familia zao. Ndiyo kusema utani michezoni unaweza kutumika kusukuma ajenda za maendeleo.
Mtafiti M Muya anasema kuwa kizuri kina kasoro zake, mara nyingi utani huu unaweza kutumia muda mwingi na pengine hata muda wa kazi. Hilo linaweza kusababisha kuzorotesha kazi.
“Kizuri ni kwamba utani wa mpira mara nyingi unalingana na utani wa wanaume ambapo unatumia makelele, kwa hiyo ni vigumu kufanyika sehemu ambapo panahitaji utulivu. Mara nyingi unafanyika wakati wafanyakazi wanaingia ofisini, wakati chai na chakula cha mchana na wakati wa kutoka kazini.”
Katika maeneo ya kazi watumishi wanaweza kuomba ruhusa ya kwenda dukani na huko ukutana kuendeleza utani huu, hapo jambo hilo linaweza kuingizia hasara kiwanda/shirika/taasisi.
Lakini pia kufanya kazi kwa pamoja kwa watumisni wanaoshabikia timu mbili tofauti inaweza kuleta kuzorota kwa kazi maana muda wote watakuwa wakishindana. Huku wanaoshauri wafanyakazi wanaoshabikia timu moja wanaweza kuwa wavivu zaidi kwani kama timu yao imefungwa basi siku hiyo uzalishaji unaweza kuwa chini, huku wakiteteana mno kwani ni watu wa kundi moja.
Ndiyo maana mimi binafsi ninashauri maafisa utumishi wanawajibu wa kutambua ushabiki wa watumishi na wanapowapangia kazi fulani kama ni kundi la watu zaidi ya 20 hakikisha nusu ni Simba na nusu ni Yanga. Kama ni Manchester United na arsenal pia wao ni nusu kwa nusu. Fanya zoezi hilo kwa siri bila ya wenyewe kufahamu hilo hili kazi ifanyike vizuri.
Mwanakwetu kwa hiyo huo ndiyo utani pahala pa kazi(utani mgudini) ambayo ilikuwa ni aina ya nne ya utani kazini.
Nakutakia kazi njema.