******************
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP – Ulrich Matei leo tarehe 25.02.2022 kuanzia majira ya saa 04:00 asubuhi katika ukumbi wa Mkapa – Sokomatola Jijini Mbeya amefanya kikao kazi na Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Wakaguzi Kata wa Jeshi la Polisi walipangwa kazi katika kata mbalimbali za Wilaya ya Mbeya.
Akizungumza kwenye kikao hicho Kamanda Matei ameelezea lengo mahususi la kikao kuwa ni kuwatambulisha wakaguzi wa kata kwa maafisa tarafa na watendaji wa kata Pamoja na kuomba ushirikiano ili lengo la Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Simon Nyakoro Sirro la kuzuia, kudhibiti matukio ya uhalifu Pamoja na migogoro ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ni chanzo cha matukio ya uvunjifu wa amani litimie kwa kuhakikisha uhalifu unakwisha.
Aidha kamanda Matei ametumia kikao kazi hicho kueleza majukumu ya msingi ya mkaguzi kata kuwa ni pamoja na kushirikiana na vikundi vya ulinzi wa kujitolea kama Sungusungu na Makampuni binafsi ya ulinzi yaliyo katika maeneo yao, kuhamasisha kuanzishwa kwa mpango wa Ulinzi Jirani katika maeneo yao, kubaini aina ya makundi ya kijamii yaliyopo katika maeneo yao na kuelewa yalipo ambapo watayatembelea na kufanya majadiliano juu ya kero yalizonazo ili kuyapatia ufumbuzi.
Majukumu mengine ni kutoa ushauri wa kisheria na kuelimisha masuala mbalimbali yanayoitatiza jamii ili kuondoa hofu miongoni mwa jamii. Pia watakuwa na jukumu la kuratibu mafunzo ya ulinzi na usalama yatakayoendeshwa katika kata zao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya Mhe.Vicent Mbua amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuleta wakaguzi kata na kuahidi ushirikiano wa dhati. Aidha ametoa maelekezo kwa watendaji wa kata kuhakikisha wakaguzi wa kata wanapatiwa ofisi, wanashirikishwa kwenye vikao vya kata na kupewa ushirikiano.