……………………………………………………………
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amewataka watendaji wa sekta ya maji kuzingatia weledi na miongozo ya Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maji.
Amesema kwa sasa kazi inaendelea na inaridhisha kwa mwenendo wake ila watendaji wasijisahau na kuharibu yaliyo mema.
Waziri Aweso amesema hay wakati wa uzinduzi wa matokeo ya tathmini ya utendaji programu ya Lipa kwa matokeo ( Pay by Result) awamu ya 6 (PbR6) naLipa kutokakana na Matokeo, (Pay for Result awamu ya Pili (PforR2).
Aidha, Aweso ametumia dakika 30 kuendesha kikao na Menejimenti ya Wizara ya Maji, na taasisi zake ikiwamo, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mabonde ya Maji, Mamlaka za Maji na Chuo cha Maji.
“Kwa dhati ya moyo wangu niwapongeze watendaji wa sekta ya maji. Tulikotoka hali ya utekelezaji wa miradi ya maji ilikuwa mbaya, Kwa sasa kuna mabadiliko makubwa. Niwapongeze na kuwatia moyo kwamba sisi viongozi wenu tuko bega kwa bega na nyinyi.” Waziri Aweso amesema.
Amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo kwa kutambua jitihada za watendaji wa sekta hiyo na kuwapa motisha ili kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi vijijini.
Amesema uamuzi wa kuanzisha RUWASA Julai 2019 umeleta tija kubwa katika sekta ya maji kwani kwa muda mfupi sana matokeo ya utendaji yameonekana. Miradi iliyokuwa imekwama kabla ya kuanzisha kwa RUWASA imekwamuliwa.
Aidha, amesisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ana matumaini makubwa ya kuondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa Watanzania kupitia rasilimali watu aliyo nayo ndani ya Wizara ya Maji.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesisitiza ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za sekta ya Maji.
“ Tuendelee kusadiana kutimiza majukumu yetu. Tufahamu kwamba sisi sote ni Wizara ya Maji bila kujali kwamba huyu ni RUWASA, huyu ni Mamlaka ya Maji au Bonde la Maji. Hakikisha kila wakati unachukua hatua mambo yote yaende vizuri” Amesema Mhandisi Mahundi
Katika tukio hilo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba amesisitiza umuhimu wa kutunza takwimu ili kuweza kufanya maamuzi yaliyosahihi katika kutoa huduma kwa Umma.
“Watumishi wa sekta ya maji mhakikisha mnakusanya, mnachakata mnahifadhi na kutoa takwimu sahihi kwa ajili ya mipango ya wizara. Eneo la Takwimu ni eneo muhim ambalo linaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupanga mipango ya Wizara.”
Kufuatia matokeo ya tathmini, Waziri Aweso ametoa zawadi kwa Watendaji mbalimbali wa RUWASA katika ngazi ya mikoa na wilaya zilizofanya vizuri katika program tofauti tofauti ambapo mkoa wa Tabora umeongoza kwa upande wa program ya PforR2 wakati Njombe ikiongoza kwa program ya PbR6